Wednesday, 26 October 2016

Vyuo vikuu waanza kupata mikopo

AKAUNTI za wanafunzi wa vikuu nchini zitakuwa zimeanza kunona baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kusema kuanzia jana imeanza kuingiza fedha za wanafunzi wote wa elimu ya juu ambao wamekidhi vigezo vya kupatiwa mikopo.
Wanafunzi 20,183 kati ya wanafunzi 58,010 ambao wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ndio ambao wamepangiwa kupata mikopo na bodi hiyo baada ya kutimiza vigezo vyote vilivyowekwa.
“Napenda kuwahakikishia waombaji kuwa boom limeanza kuingia leo, kwa kuwa fedha hizo zinapitia benki baadhi wanapata kesho na wengine siku zinazofuata, ila sisi tumeshatimiza wajibu wetu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru wakati akizungumza na gazeti hili jana.
Kwa idadi hiyo ya wanufaika wa mikopo iliyotangazwa na bodi, ni wazi kuwa wanafunzi wengine 37,827 hawatapatiwa mkopo kutokana na kukosa sifa ambao zimeainishwa na bodi hiyo.
Jumla ya wanafunzi 88,163 waliomba mikopo ya HESLB.
Badru alifafanua kuwa miongoni mwa waliokosa mikopo ni waombaji walioomba wakati wana umri wa zaidi ya miaka 30 na wengine wamekosa sifa za kukopeshwa kwa kuwa hawakuomba kabisa.
“Kuna wanafunzi kama 90 wamekosa mikopo kwa sababu ya umri wao kuwa mkubwa, sisi tunatoa mikopo kwa wanafunzi wanaotoka sekondari. Pia kuna wanafunzi wengine kama 6,561 hawakuomba kabisa mikopo licha ya kudahiliwa na TCU hao nao tunasema hawana sifa ya kukopeshwa,” alisema Badru.
Hata hivyo, kuna nafasi za wanafunzi 5,534 ambazo zimeachwa na bodi hiyo kwa ajili ya waombaji waliochelewa kupata udahili au kwa wale ambao wamekosa mikopo halafu wakakata rufaa na kushinda.
Katika ufafanuzi wa waliopata mikopo, Badru alisema kati ya wanafunzi hao yatima waliopata mkopo ni 873, wenye ulemavu wa viungo wako 118, wahitaji wenye mzazi mmoja 3,448, waliofadhiliwa na taasisi mbali mbali 87, wahitaji wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na Wadahiliwa wahitaji wanaosoma kozi zingine ni 9,867.
Badru pia alisema wanafunzi wengine 93,295 ambao wanaendelea na masomo yao, nao wameshaingiziwa fedha zao kwa utaratibu uliowekwa wakati wanapatiwa mikopo yao ya awali. Bajeti ya Serikali iliyoidhinishwa kwa ajili ya ukopeshaji kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ni Sh bilioni 483.
“Ila baada ya kuwapatia mikopo hiyo tutaendelea na uhakiki kubaini wale ambao walijaza taarifa ambazo sio sahihi na pia tunataka kuona anayepata mkopo ni mwanafunzi mwenye sifa tu,” alisema Badru.
Alifafanua kuwa baada ya hatua hiyo wanufaika wote wanaopungukiwa na sifa watachunguzwa kwa ajili ya kurekebishiwa au kuondolewa katika unufaika wa mkopo.
Pia waombaji waliowasilisha taarifa zenye upungufu, taarifa zao zitahakikiwa, na wakibainika kuwasilisha taarifa za uongo watachukuliwa hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kufutiwa mikopo yao. Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa wanufaika wote watatakiwa kuhuisha taarifa kwa kujaza dodoso.
Taarifa za ziada za kiuchumi za wazazi au walezi wao zitatumika kutanua uhalisia. Wale watakaokutwa na hadhi zisizo stahili, watapoteza sifa za kuendelea kupata mikopo na kulazimika kurejesha kiasi watakachokuwa wamepokea tayari.
Juzi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifunga maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo na akasema kufikia leo Alhamisi asilimia 90 ya waombaji waliotimiza masharti wawe wameshalipa fedha zao.
Aliwataka watumishi wa bodi ya mikopo kutimiza wajibu wao kuhakikisha kwamba kwa wale ambao uhakiki wao umekamilika wapatiwe mikopo hiyo kwa wakati.
Alisema kamwe serikali haitawavumilia watumishi ambao watachelewesha kwa makusudi mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Pia aliagiza kuwa kama kuna tatizo juu ya utoaji wa mikopo, taarifa itolewe ndani ya serikali haraka ili ifanyiwe kazi kuzuia mgogoro kati ya wanafunzi na serikali yao.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog