Wednesday, 26 October 2016

NSSF hatarini ‘kulizwa’ bil 270/-

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa linaweza kupoteza kiasi cha Sh bilioni 270, zilizoingizwa kwenye mradi wa ubia baina yake na Kampuni ya Azimio Housing Estates (AHEL), kama shirika hilo lisipokuwa makini.
Pamoja na hayo, kamati hiyo baada ya kubaini madudu kadhaa katika hesabu za shirika hilo, imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu wa mikopo yote iliyotolewa na NSSF kwa vyama vya akiba na mikopo.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mradi huo ambao ni ujenzi wa mji wa kisasa katika eneo la Dege Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema kwa sasa kinachoangaliwa kwenye mkataba huo ni athari za kupoteza fedha hizo.
Profesa Kahyarara alisema pamoja na shirika hilo kuwepo kwenye ubia huo, lakini limegundua ekari zilizopo kwenye mkataba si za uhalisia.
Alisema kwa mujibu wa mkataba zilitakiwa ziwe ekari 20,000 lakini kiuhalisia baada ya kufanya tathmini zipo ekari zaidi ya 3,500.
Aidha, alifafanua kuwa bei iliyothaminiwa kwenye ekari hizo pia ni tofauti kwani mwekezaji huyo alithaminisha ardhi hiyo kwa Sh milioni 800, lakini baada ya NSSF kufanya uchunguzi wake ikabaini kuwa ekari moja thamani yake ni Sh milioni 25.
Kwa mujibu wa taarifa za CAG zinaeleza kuwa NSSF iliingia ubia na kampuni hiyo na kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Builders Limited.
Katika mkataba huo, Azimio Housing Estates itatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Kigamboni kupitia mradi uliopo eneo la Dege.
Hata hivyo, mradi huo umesimama utekelezaji wake tangu Februari, mwaka huu kutokana na mwekezaji kutokuwa na fedha huku NSSF tayari ikiwa imeshaingiza Sh bilioni 270.
Katika ubia huo, NSSF inamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estates inamiliki asilimia 55 ya hisa na jumla ya gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 653.44.
Kwa mujibu wa utaratibu wa uchangiaji mtaji, NSSF itatoa fedha zenye thamani ya asilimia 45 ya gharama za mradi na Azimio itatoa fedha zenye thamani ya asilimia 35 ya gharama za mradi pamoja na ardhi ambayo itathaminishwa kuwa asilimia 20 ya gharama za mradi.
Kutokana na hali, Profesa Kahyarara alisema kwa sasa unafanyika ukaguzi maalumu kwenye miradi yote ya NSSF ikiwemo mradi huo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti hatuwezi kwa sasa kutoka kwenye ubia huu tunaweza kupoteza fedha hizo, lazima tuwe makini ili kuhakikisha mwekezaji huyo Azimio anarejesha fedha hizo,” alisisitiza mkurugenzi huyo.
Akihoji kuhusu utata uliojitokezakwenye ripoti ya CAG kuhusu mradi huo, mbunge wa Msalala Ezekiel Maige, alibainisha kuwa mradi huo umegubikwa na uchafu.
“Tukubaliane tu mradi huu umegubikwa na madudu, kwa nini usivunjwe na una uhakika gani utakuwa safi NSSF ikiendelea kuwa kwenye huo mkataba tena? Alihoji Maige.
Naye Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ali alisema kwa taarifa zilizopo kampuni hiyo ya Azimio ilitaka kukopa NSSF wakati ina tayari ina deni katika shirika hilo, huku ikiwa haijaingiza fedha zozote katika mradi huo wa ubia.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly alitahadharisha kuwa kwa sasa mkandarasi wa mradi huo yupo eneo la mradi, hivyo kuna uwezekano wa kupoteza fedha nyingi zaidi endapo fedha zilizowekezwa tayari na NSSF hazitorejeshwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba alihoji ni kwa nini Azimio imeingia ubia tena katika kutekeleza mradi wa Mji wa Kisasa wa Arumeru na kupewa kazi nyingine ya kuwa mhandisi mshauri wakati utekelezaji wake ni mbovu.
Alihoji NSSF ina mkakati gani wa kurejesha kiasi cha Sh bilioni 43.9 zilizolipwa kwa kampuni hiyo ya Azimio kwa kazi ya ushauri ambayo lengo lake halijatimia.
Kuhusu suala la mikopo, PAC imeagiza ufanyike ukaguzi maalumu wa mikopo yote iliyotolewa na shirika hilo kwenye Saccos, baada ya kubainika kuwa Saccos ya Bumbuli ilipatiwa mkopo wa Sh bilioni 2.4 ndani ya mwaka mmoja.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alitoa agizo hilo kwa CAG na kusisitiza kuwa kitendo cha Saccos ya Bumbuli kupatiwa fedha hizo ndani ya mwaka mmoja kimewashtua wajumbe wa kamati hiyo. Kaboyoka alisema maelekezo mengine kuhusu suala hilo yatatolewa bungeni kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge 117(10).
Awali wakichangia wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mbunge wa Kilindi, Omar Kigua alihoji vigezo vilivyotumika mpaka Saccos moja kupewa mkopo mara tatu. Alifafanua kuwa kwa mujibu wa ripoti ya CAG, NSSF imetoa mikopo kwa SACCOS tisa kiwango kinachozidi asilimia 50 ya thamani ya mali za Saccos husika kinyume cha Sera ya kukopesha ya shirika hilo.
Katika ripoti ya CAG mbali na Bumbuli pia Saccos zingine zilizopatiwa fedha nyingi ni Korongo Amcos Saccos, UMMA Saccos, SBC Saccos Ltd, Hekima Saccos, Ukombozi Saccos Ltd, Uzinza Saccos Ltd, Harbour Saccos, na Umoja Saccos.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe alisema kwa sasa bodi imesimamisha mikopo kwa Saccos zote hadi uchunguzi ukamilike na utawekwa utaratibu mpya wa utoaji mikopo.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog