Thursday 27 October 2016

Historia MOI upasuaji kwa wenye kibiongo

KIBIONGO ni tatizo la kupinda kwa mgongo upande moja hasa wa kulia, hali inayomfanya mtu aliye na hali hiyo kutembea akiwa ama ameinama au kujikunja. Tatizo hilo mtu huweza kuzaliwa nalo au kutokea baadaye mtoto anapokuwa amefikisha umri wa miaka mitatu na kuendelea.
Kwa kuwa hapa nchini kulikuwa hakuna upasuaji kwa tatizo hilo, watu waliokuwa na shida hiyo walikuwa wakikua nalo hivyo hivyo isipokuwa wenye uwezo wa kifedha na kuwa na taarifa sahihi walipelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. Hivi sasa ufumbuzi umepatikana nchini.
Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji mkubwa kwa mafanikio wa kunyoosha mfupa wa mgogo wa mtoto uliopinda (kibiongo). Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma anasema upasuaji huo umefanyika kwa kutumia teknolojia ijulikanayo kama ‘posterior instrumentation and fusion’.
Inahusisha uwekaji wa vyuma maalumu kwenye mfupa wa mgongo katika sehemu ya juu na chini ya mfupa wa mgongo na kuufanya unyooke kama inavyotakiwa.
Dk Othman anasema taasisi hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji huo kupitia madaktari bingwa walioko kwenye mafunzo ya ubobezi wa juu katika upasuaji wa mifupa na mgongo kwa watoto kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Marekani.
“Uanzishwaji wa upasuaji huu umetokana na kuanzisha ushirikiano wa kimafunzo kati ya Taasisi ya MOI na Chuo cha Madaktari bingwa wa upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA) na madaktari bingwa kutoka Marekani,” anasema.
Anasisitiza kuwa uanzishwaji huu wa kunyoosha migongo ya watoto iliyopinda unatarajiwa kuisaidia serikali kupunguza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi ambazo ni za gharama kubwa.
Kutokana na hatua hiyo, uongozi wa MOI unatoa mwito kwa madaktari wote nchini kwenda kupata mafunzo hayo kwenye taasisi hiyo. Pia wazazi wenye watoto wenye matatizo hayo wawapeleke hospitalini wafanyiwe uchunguzi na upasuaji.
Awali watoto waliokuwa wakienda India na sehemu nyingine kutibiwa iliwagharimu dola 6,000 (Sh milioni 13 na zaidi).
“Sasa hivi upasuaji huo unafanyika hapa nchini, mgongo unanyooka na mgonjwa anarudi katika hali ya kawaida kwa gharama ya dola 2,000 tu (takribani Sh 4,400,000),” anasema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Viungo, Bryson Mcharo anasema huo ni upasuaji mpya, na ni mara ya kwanza kufanyika MOI lakini umekuwa ukifanyika nchi nyingine.
Anasema ukubwa wa kupinda kwa mgongo huo hutegemeana na umri wa mtoto. Anasema wataalamu hawajabaini sababu ya tatizo hilo. Mcharo anasema hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika upasuaji huo, na hivi sasa yupo kwenye mafunzo ya upasuaji wa mifupa ya watoto.
Katika upasuaji uliofanyika nchini, anasema walifanikiwa kunyoosha mgongo wa mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma kidato cha kwanza. Anasema kwa sasa Moi wana vifaa vinavyowawezesha kuwawekea wagonjwa 30 baada ya kufanyiwa upasuaji.
Inaelezwa kwamba baada ya mtu kufanyiwa upasuaji huo na kuwekewa kifaa maalumu mgongoni, kuna baadhi ya vitu hataweza kuvifanya tena kama awali.
Hupewa masharti ya kutoinama endapo anataka kuokota kitu ama kupinda kama wengine wanavyoweza na pia huelekezwa namna ya kuishi na kifaa hicho mwilini. Mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Yombo, Temeke, Dar es Salaam, Itika Mwankenja anasema mtoto wake hakuzaliwa na tatizo hilo na kwamba lilimpata akiwa na umri wa miaka 11.
“Kama wazazi tuligundua hali hiyo ya mabadiliko kwa mtoto wetu kwa kuwa ni kitu ambacho hatukuwahi kukiona kwake,” anasema.
Mzazi huyo anamshukuru Mungu kwa kumwezesha mtoto wake kufanyiwa upasuaji mkubwa wa mafanikio. Kwa mujibu wa mama huyo hivi sasa kuna tofauti kubwa kabla ya upasuaji na baada ya mtoto kufanyiwa upasuaji huo.
Anasema mtoto wake huyo anaendelea vizuri na mazoezi anayoyafanya baada ya upasuaji huo. Mtoto huyo anayesoma kidato cha kwanza anasema baada ya kupatwa hali hiyo, alikuwa akichoka anapokaa kwa muda mrefu hasa akiwa darasani.
“Ilibidi niwe najikaza ili muda wa kurudi nyumbani ufike na nilikuwa ninaandika kwa shida lakini kwa sasa baada ya upasuaji naweza kukaa muda mrefu,” anasema.
Ni dhahiri kwamba, MOI imeandika historia mwaka huu ya kufanya upasuaji mkubwa wenye mafanikio, hatua inayotajwa kuwa ni ukombozi kwa jamii ya Tanzania na majirani zetu.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog