Monday, 5 September 2016

TRA YAFUNGA AKAUNTI ZA MSALABA MWEKUNDU

HALI imezidi kuwa tete ndani ya Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzifunga akaunti zaidi ya nne za chama hicho kutokana na kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi ya makato ya mshahara wa wafanyakazi (PAYE).
Taarifa kutoka ndani ya TRCS zinaeleza kuwa kodi inayodaiwa na TRA ni ile ya PAYE ya wafanyakazi zaidi 200 wanaofanya kazi mkoani Kigoma katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2011/2015.
Kodi hiyo inakadiriwa kufikia shilingi milioni 790 huku chama hicho kikidaiwa pia shilingi bilioni 1.5 malimbikizo ya kodi ongezeko la thamani (VAT) na mapato kutokana mauzo ya magari.
Hali ndani ya TRCS imeelezwa kuwa mbaya kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kujitumbukiza katika vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa TRA imechukua uamuzi wa kufunga akaunti hizo baada ya kufanya mawasiliano ya muda mrefu na uongozi wa chama hicho ambao hata hivyo, ulishindwa kulipa malimbikizo ya kodi hizo.
Raia Mwema imebaini kuwa akaunti zilizofungwa zipo katika benki ya NBC Ltd tawi la Kigoma, benki ya CRDB tawi la Kigoma na nyingine iliyopo benki ya NMB tawi la Kasulu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa pia akaunti za chama hicho zilizopo katika benki mbili kubwa jijini Dar es Salaam zimefungwa ikiwa ni hatua zaidi za TRA kuibana chama hicho.
Taarifa za ndani zaidi kutoka TRCS na uthibitisho wa nyaraka mbalimbali zinaeleza kuwa fedha hizo za makato ya kodi ya PAYE zilitumiwa kifisadi na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Sakata hilo la TRCS kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi hiyo lilianza mwanzoni mwa mwaka huu hasa baada ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu tano ambayo imekuwa ikisisitiza na ikisimamia kwa weledi ulipaji wa kodi.
Mei 30 mwaka huu Kaimu Katibu Mkuu wa TRCS, Peter Mlebusi, alimwandikia Waziri Fedha, Dk. Philip Mpango, kwa barua yenye kumbukumbu namba TRCS/T/1/264  akimwomba waziri huyo kwa mamlaka yake kufuta deni la malimbikizo ya kodi hizo.
Hata hivyo maombi hayo ya TCRS yalijibiwa Juni 21 mwaka huu kwa barua yenye kumbukumbu namba CAB.481/547/01 kutoka Wizara Fedha kuwa hakuna mamlaka ya kisheria kwa chama hicho kusamehewa kulipa malimbikizo ya kodi hiyo.
Barua hiyo ambayo imesainiwa na Doto M. James kwa niaba ya Katibu wa Wizara hiyo, imebainisha kuwa TRCS ni lazima walipe kodi hiyo kama sheria inavyoelekeza kwa kuwa maombi yote ya kusamehewa  kodi kwa kawaida hupitishwa kwa tangazo katika gazeti la serikali (GN).
Pamoja na barua hiyo ya Wizara, TRCS waliendelea kung’ang’ania kutolipa kodi hiyo ambapo Kaimu Katibu Mkuu Mlebusi alimwandikia barua nyingine Kamishna Mkuu wa TRA, Julai 18 mwaka huu, kuwa chama hicho kisamehewa kulipa riba ya shilingi 279,543,521.74.
Kwa mujibu barua hiyo yenye kumbukumbu TRCS/T/1/267, Mlebusi anadai kuwa kodi wanayodaiwa ni shilingi 510,848,086.85  na chama hicho ni chama  hiari (charitable organization) hivyo hawatengenezi faida.
Kutokana na mvutano huo wa muda ndipo wiki iliyopita TRA walipofanya uamuzi wa kufunga akaunti za chama hicho hatua ambayo imetajwa kuathiri shughuli za chama hicho kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na Raia Mwema Jumanne wiki hii, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRCS aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema kufungwa kwa akaunti hizo kunahatarisha chama hicho kutimiza malengo yake.
 “Hali hii inatishia malengo ya chama ambayo ni kusaidia jamii pale inapopatwa na majanga ya kibinadamu yanayosababishwa na vita, maradhi au majanga ya asili,” alisema mjumbe huyo.
Mjumbe huyo aliongeza kuwa hatua hiyo pia imechafua taswira ya chama hicho mbele ya jamii ya kimataifa hivyo kuna uwezekano mkubwa wafadhili kusitisha misaada yao hatua ambayo itaathiri wananchi wanaokabiliwa na majanga mbalimbali ambao wanapata misaada kupitia TRCS.
"Mamlaka za serikali kama Takukuru na ofisi ya rais ambaye ndiye mlezi wa chama wanatakiwa kuchunguza haraka ufisadi wa viongozi wa juu na matumizi mabaya ya madaraka ili kuinusuru taasisi ambayo ni nyeti sana kwa maslahi ya nchi yetu," aliongeza
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba