Thursday, 27 October 2016

Mfumo wa PReM utakavyodhibiti wanafunzi hewa

TANGU serikali iliporuhusu mazingira ya soko huria katika sekta ya elimu, kumekuwapo na shule binafsi nyingi. Katika shule hizo binafsi, suala la kuhamisha wanafunzi limekuwa halizingatiwi kama ilivyokuwa miaka ya nyumba ambapo ilikuwa ni lazima taarifa za mwanafunzi za kuhama zipate baraka na mamlaka za elimu katika ngazi za kata, wilaya na mkoa na taarifa kubaki katika ngazi hizo.
Kukatika kwa mnyororo huo ulifanywa uhamishaji na taarifa za mwanafunzi kutokuwepo katika ngazi husika zaidi ya shule ambayo mwanafunzi husika anatoka na kuhamia. Badala yake shule ambayo imepokea mwanafunzi ilikuwa ikiandika barua Necta ya kuainisha wanafunzi waliohamia na shule walizotoka.
Ili kuwa na mfumo unaoeleweka, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limeunda mfumo wa kutunza taarifa za wanafunzi wa Shule za Msingi (PReM) ambao utasaidia katika uandikishaji wa wanafunzi wote wa shule za msingi na wanafunzi hao kupewa namba maalumu itakayomtambulisha mwanafunzi katika ngazi mbalimbali za mafunzo zinazosimamiwa na baraza.
Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi anasema mbali na mfumo huo kumtambulisha mwanafunzi, pia utasaidia katika uhamisho wa mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine ndani na nje ya mkoa katika shule za umma na zile binafsi.
“Ni mfumo ambao utarahisisha utaratibu unaotumika sasa wa kuhamisha mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine ili kuondoa tatizo la wanafunzi hewa,” anasema. Anasema Mfumo wa PReM utasaidia katika uandaaji na utoaji wa takwimu za wanafunzi katika ngazi ya shule, wilaya, mkoa hadi ngazi ya kitaifa.
Aidha, Nchimbi anasema mfumo huo pia utasaidia katika ufuatiliaji wa taarifa za matokeo ya kila mwanafunzi kuhakikisha wadau mbalimbali wa elimu wanapata ufahamu wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya shule.
Baraza limefanya majaribio ya mfumo huu katika mikoa miwili ya Mwanza na Ruvuma na ifikapo Desemba mwaka huu, utaimarishwa ili Januari hadi Mei 2017, utumiwe na mikoa yote kusajili wanafunzi wa shule za msingi.
“Mfumo huu wa PReM utasimikwa Baraza la Mitihani Tanzania na kutumiwa na wadau mbalimbali wa Elimu. Baraza la Mitihani la Tanzania litahakikisha mfumo huu unapatikana katika ngazi za wilaya ili wadau wote waweze kupata taarifa mbalimbali za elimu,” anasema.
Anasema NECTA ina wajibu wa kutoa mafunzo ya uendeshaji wa mfumo wa ngazi ya mkoa, kuandaa na kusimamia taratibu za uandikishaji na utunzaji wa taarifa za mwanafunzi katika ngazi ya wilaya na mkoa, na kuchukua taarifa za usajili za wanafunzi wa darasa la nne na la saba.
“Necta pia ina wajibu wa kuweka matokeo ya mitihani ya kitaifa, kutatua changamoto za mfumo wa PReM katika ngazi ya mkoa, kuhakikisha usalama wa taarifa zilizohifadhiwa katika mfumo na kusimamia uendeshaji wa mfumo katika ngazi zote.
Aidha, Nchimbi anasema ili kufikia malengo mahususi ya mfumo wa PReM, kila mdau wa elimu atatakiwa kutimiza wajibu wake. Wadau hao ni mwalimu mkuu, mratibu wa elimu kata, ofisa elimu wilaya, mkoa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Anasema kwa ofisi ya mwalimu mkuu, inawajibu wa kuandaa orodha ya wanafunzi kwa ajili ya kuandikishwa kwenye mfumo wa kupeleka wilayani, kupeleka taarifa za uhamisho na matokeo ya kila mwaka kwa wanafunzi wote wilayani na kupokea ripoti za uandikishwaji na uhamisho wilayani.
Nchimbi anasema kwa upande wa ofisi ya mratibu wa elimu kata, ina wajibu wa kutoa ripoti za takwimu za shule katika kata husika, na kusimamia uingizaji wa taaria za wanafunzi ngazi ya shule na kata.
“Ofisi ya Ofisa Elimu wilaya yenyewe ina wajibu wa kusimamia uingizaji wa taarifa ya uandikishwaji, uhamisho na matokeo kwenye mfumo, kuthibitisha uhamisho wa mwanafunzi kwenye mfumo na kutoa ripoti za takwimu za shule zote wilayani.
Nchimbi anasema ofisi ya elimu mkoa, wanawajibu wa kutekeleza mfumo wa PReM kwa kusimamia uandikishwaji wa wanafunzi wa shule zote katika mkoa husika, kuthibitisha uhamisho wa mwanafunzi katika shule zote za mkoa husika na kutoa ripoti za takwimu za shule za mkoa husika.
Anasema kwa upande wa Ofisi ya Rais, Tamisemi inawajibika kuhakikisha kila mkoa unaingiza taarifa za wanafunzi wa ngazi zote katika shule za msingi na kutoa ripoti mbalimbali za takwimu na matokeo kulingana na mahitaji yao.
Nchimbi anasema wanawajibika pia kupokea na kuingiza taarifa za uandikishaji kutoka shule za wilaya na kuingiza taarifa za matokeo na uhamisho kwenye mfumo na kutoa ripoti za uandikishaji na uhamisho za kila shule katika wilaya husika.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog