Thursday, 27 October 2016

Polisi yawashikilia wanne mtandao wizi wa magari

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za wizi wa magari kwa kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema jana Dar es Salaam kuwa askari waliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Watuhumiwa hawa wanajihusisha na wizi wa magari kwa mbinu ya kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima, pamoja na kukata vibali vya namba ya ‘chassis’ ya magari hayo kisha kuweka kwenye magari waliyoyaiba,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema baada ya askari kupata taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji eneo la Tandale na kukamata mtuhumiwa Dennis Gasper (25), mfanyabiashara wa Manzese Uzuri akiwa na mabaki ya gari namba T 290 DDM Toyota ALPHAD.
Alisema katika mahojiano mtuhumiwa alitaja watuhumiwa wengine na kuwaongoza askari hadi Magomeni Mikumi maeneo ya kituo cha daladala na kuwakamata watuhumiwa wengine watatu ambao ni Alfred Ditrick (33), mkazi wa Sinza, Venance Bureta (24) wa Mbezi na Dickson Valentino (23) mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na mkazi wa Kimara, wote katika Jiji la Dar es Salaam.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikutwa na gari la wizi namba T 368 CES Toyota Passo na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya wizi wa magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuyauza nje ya mkoa huo.
Katika tukio lingine, askari wamekamata magari mengine matatu ya wizi yaliyoibwa mkoani Dar es Salaam na kupelekwa mafichoni Arusha yakiwemo Toyota Vitz T 262 CTF, Suzuki Carry lenye namba za usajili T 935 CPC, Toyota Passo lenye namba za usajili T 368 CES na Toyota Landcruiser Prado lenye namba za usajili T 735 BLZ.
Alisema watuhumiwa wa mtandao huo wanashikiliwa mkoani Arusha na juhudi za kuwafuata zinafanyika ili kuja kuwaleta Dar es Salaam kujibu mashitaka yanayowakabili.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog