Wednesday, 26 October 2016

Magufuli ni yule yule tuliyemchagua

"NYOTA yake kisiasa ilianza kung’aa mapema zaidi katika viunga vya Tanzania akianzia na utumishi wa umma hadi kufikia ngazi ya uwaziri. Umri wake umeingia katika utu uzima na kuanza kugusa uzuri wa nywele zake, lakini katika mwili wake bado nguvu ya ujana ipo."
Sentensi hiyo ilikuwa kwenye makala iliyowahi kuchapishwa katika gazeti hili, ambapo mchambuzi kutoka Zanzibar, Juma Mohammed, alitabiri mengi ambayo Magufuli anayafanya sasa akiwa Ikulu.
Juma alidokeza kwamba ushiriki wake katika shida za watu na uchapakazi akiwa waziri katika wizara mbalimbali na mbunge wa Jimbo la Chato, ni hali aliyoanza kumtofautisha na wagombea wengine, iwe ni wa vyama vya upinzani au wa chama chake, Chama Cha Mapinduzi.
Katika kipindi cha uwaziri wake na ubunge, Dk John Magufuli alikaa kwa wema, hisani na adabu na wananchi wenzake na ndio maana haikustajaabisha kuona Watanzania wengi, wa kike, kiume, vijana kwa wazee wakamuunga mkono kumpigia kura Oktoba 25 mwaka jana na hata sasa wanaendelea kumuunga mkono kwani ndio tegemeo lao.
Tuliokuwa tukifuatilia hotuba zake wakati akiwa Mgombea Urais wa CCM, Dk Magufuli, kwa hakika maneno yake yalipenya vyema kwenye masikio, yakaakisi shauku ya mabadiliko ya kweli na siyo ya 'kuzungusha mikono'.
Kuna waliodhani ni porojo zilizozoelekwa kwa wanasiasa na ambazo tulizisikia pia kwenye majukwaa ya wagombea wa upinzani lakini wanaomjua vyema Magufuli hawakuwa na mashaka na ahadi zake na kwa hakika wananchi walianza kushuhudia ukweli wa ahadi zake mara tu alipoanza kazi ya kuongoza nchi hii baada ya kuapishwa.
Kutokana na hulka yake tangu akiwa Waziri, Dk Magufuli hakuwa mtu wa porojo, ubabaishaji na usanii na ndio maana alipoibuka na kaulimbiu ya 'Hapa Kazi tu' wakati wa kampeni, watanzania walimwelewa na wakampa kura zao kwa wingi Oktoba 25 na kwa hakika sasa wanaona kazi inafanyika. Juma katika andiko lake anasema:
"Watu wenye busara na waadilifu mara nyingi wanawatendea wema binadamu wenzao katika nchi na kwa hakika maisha yanakwisha kwa mtu huyo kukumbukwa na jamii kwa wema wake, lakini wapo pia ambao hukumbukwa kwa maovu na ubaya wao, ufisadi na kuifisidi nchi".
Hakuna ubishi kwamba Dk Magufuli ni miongoni mwa watu wema na yale ambayo ameyafanya Ikulu katika kipindi kifupi yanadhihirisha kwamba Dk Magufuli ni yuleyule aliyekuwa makini na imara akiwa waziri na sasa akiwa mkuu wa nchi.
Ni kwa muktadha huo, kama alivyotabiri Juma katika uchambuzi wake, Dk Magufuli ataingia katika orodha ya watakaoacha simulizi ya uchapakazi, uadilifu, upendo, umoja na mshikamano kwa jamii ya Tanzania kwa ujumla wake.
Ndio maana, Profesa Patrick Lumumba wa Kenya, hasiti kueleza hadharani namna anavyomkubali rais wetu akisema kwa sasa ndiye rais pekee wa Afrika ambaye anaonekana amekwenda Ikulu kuwatumikia wananchi na si kutafuta mambo mengine.
Wakati akiwa na miezi michache tu ofisini, Profesa Lumumba aliwahi kusema katika mahojiano kwamba Magufuli ni "real deal", akimaanisha kwamba anayofanya si nguvu ya soda bali ndivyo alivyo kwa maana ya utumishi wa umma uliotukuka.
Kwa mwenendo wake ambao unaonesha haukwazwi na madaraka makubwa aliyo nayo sasa, bila shaka rais huyu wa awamu ya Tano ataendelea kuwa nguzo na hazina ya utawala uliotukuka kwa bara la Afrika, lakini pia atakuwa chachu ya mabadiliko ya kweli yanayotegemewa na wananchi waliowengi.
Bila shaka katika kipindi kifupi, wapo Watanzania ambao wameshaona madhara ya kuwaunga mkono wagombea mafisadi maana ubaya wake, kama alivyoonya Juma katika andiko lake unazidi ule wa chuma kuliwa na kutu maana sumu ya maendeleo ni ufisadi.
Dk Magufuli ameipatia tunu ya neema Tanzania na faida ya kumchagua inaonekana katika kila pembe ya nchi, Afrika na sehemu nyingine ya dunia na sasa Watanzania duniani kote wanatembea kifua mbele wakijivunia kuwa na rais jembe. Hakika waliomuita tingatinga hawakukosea.
Alipoanza kuahidi kutumbua majipu, wengi hawakuamini kwamba atatakeleza kauli hiyo nzito kwa vitendo, kwani hakuna shaka kwamba baadhi ya majipu ni watu waliomfanyia kampeni, kumpigia kura au kuwa naye katika chama chake.
Magufuli ametekeleza utumbuaji majipu kwa vitendo na hivyo kuleta nidhamu katika utumishi wa umma uliokuwa umegubikwa na shombo kubwa ya utovu wa maadili, watu wakijifanyia mambo wanavyotaka, wakiendekeza ubinafsi wao.
Kwa hatua hiyo, sasa Tanzania inaendelea kupata watu wenye wito wa kuutumikia umma wa Watanzania na siyo matumbo yao. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema kwamba Ikulu ni mahala patakatifu na kwamba anayeingia mahala hapo anapaswa kuwafanya hata marafiki zake wajue kwamba hakwenda pale kupageuza kuwa pango la walanguzi, na bila shaka Magufuli hilo ameliweza.
Kwamba uteuzi ambao amekuwa akiufanya hauangalii sura ya mtu bali uwezo wa wale anaowateua na wateule wake wanapokwenda kinyume cha maadili hasiti kutengua uteuzi wake muda uleule.
Mwalimu Nyerere pia alipata kusema kwamba Ikulu ni mzigo na mtu mkweli kabisa kabisa hapakimbilii kwa kuwa matatizo ya wananchi ni mzigo wa huyo aliyeko Ikulu.
Kwa matendo yake na jinsi anavyopigana kuhakikisha wanyonge wa nchi hii nao wanafaidi keki ya mafanikio, hakuna ubishi kwamba Rais Magufuli analijua hilo na kulifanyia kazi.
Anajua matatizo yetu ni mzigo wake na ndio maana anahangaika kuhakikisha kwamba mapato ya nchi yanafika kunakostahili na yanatumika kwa faida ya Watanzania wote na si genge la watu wachache wenye roho za kinyang'au.
Akiwa anatimiza mwaka mmoja ofisini, hakika Magufuli amedhihirisha kwamba ni yuleyule ambaye wakati akiwa waziri tulitamani awe waziri wa wizara zote kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka.
Shime wananchi, tumuombee kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa siha na moyo wa kututumikia na pia tumuunge mkono kwa kuchapa kazi na kulipa kodi.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

Arquivo do blog