SERIKALI ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati
nchini hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya
miwa.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Balozi wa Brazil nchini,
Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo naye.
Balozi Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake ina ujuzi na
uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo
mbalimbali hususan maji.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya viwanda, unahitaji
umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba
Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda
mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha
umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.
Alitaja eneo lingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni
uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa
chanzo kizuri cha nishati safi.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa
Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo ambayo
Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa kuwekeza
Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na Serikali.
Alisema, kunaandaliwa utaratibu maalumu utakaokuwa wa wazi na
kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya kupunguza au
kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu unaotumika katika
majadiliano pasipo sababu za msingi.
0 comments:
Post a Comment