FAMILIA nane zenye watu zaidi ya 20 kwenye mtaa wa Mharakani kata ya
Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani zimenusurika kufa baada ya
moto kutokea wakati wanafamilia hao wakiwa wamelala.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, waathirika wa tukio hilo la
moto walisema lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 8, mwaka huu saa 6:30
usiku.
Mmoja wa waathirika hao, Emmanuel Mhina, alisema watu waliokuwa
jirani na nyumba yao ndio waliowafahamisha juu ya moto huo ambao
unasadikiwa ulianzia kwenye moja ya maduka yaliyo kwenye nyumba hiyo.
Alisema kuwa walikuwa wamelala lakini ilipofika saa saba kasorobo
usiku, waliamshwa na watu na walipoamka walikutana na moto mkubwa ambao
hawakujua ulianza saa ngapi ndipo walipoanza kujiokoa.
“Tunamshukuru Mungu tumenusurika licha ya mali zetu zote kuteketea
kwa moto ambao ulianzia kwenye moja ya maduka ambayo yameungana,”
alisema Mhina.
Naye Said Juma alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa kwani
amepoteza vitu karibu vyote na kufanikiwa kuokoa vichache hali ambayo
inamfanya aanze upya maisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Yahaya Abdalah, alisema kuwa
wananchi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Jeshi la Polisi
walifanikisha kuzimwa kwa moto huo.
Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege, Robert Machumbe, alisema kuwa
waathirika hao hawakuweza kuokoa kitu kwani vitu vyote viliteketea kwa
moto huo.
Katika hatua nyingine, mtoto mwenye umri kati ya miaka minne na nusu
amenusurika kufa katika moto huo baada ya mama yake kumwacha kwenye
nyumba hiyo akiwa amemfungia na kwenda kusikojulikana.
Inaelezwa kuwa, mtoto huyo aliokolewa na mwanajeshi wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye ni miongoni mwa waliounguliwa na
nyumba hiyo baada ya kujitosa kumwokoa.
0 comments:
Post a Comment