Tuesday, 9 August 2016

Manji kutinga kizimbani leo

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji leo atapanda kizimbani Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi alikoburuzwa na waliokuwa watendaji wa klabu hiyo, Selestine Mwesigwa na Luis Sendeu.
Septemba mwaka 2012, Mwesigwa akiwa Katibu Mkuu wa Yanga na Sendeu akiwa Ofisa Habari wa klabu hiyo ya Jangwani, waliondolewa katika ajira zao kwa kile kilichoelezwa kuwa utendaji mbovu.
Mwesigwa na Sendeu waliomba bila mafanikio walipwe na Yanga fidia ya Sh 262 milioni, ambapo kati ya hizo, Sendeu anadai Sh 79 milioni na Mwesigwa anadai Sh 183 milioni.
Watendaji hao walifikisha suala hilo katika Baraza la Kazi ambapo walishinda madai yao na hivyo Yanga iliamriwa kuwalipa kiasi hicho cha fedha hata hivyo fedha hizo bado hawajalipwa kitendo ambacho kimeilazimu Mahakama kumuita kwa nguvu Mwenyekti huyo wa Yanga leo bila kukosa.
Wito huo ulitolewa Juni 24, ambapo Manji ametakiwa kufika mahakamani leo Agosti 9 saa 3:00 asubuhi bila kukosa wala kutuma mwakilishi.
“Unatakiwa kufika binafsi mbele ya Mahakama hii ikikaa Dsm tarehe 9, mwezi wa nane mwaka 2016 mbele ya Mheshimiwa Ujimo na kubaki Mahakamani hadi uruhusiwe na Mahakama kuondoka kwa ajili ya kutajwa, kusikilizwa kwa marejeo/ maombi/mgogoro na unatakiwa kujibu hati ya kiapo ndani ya siku 15."
Katika kikao cha dharura cha klabu hiyo kilichokaa Jumamosi iliyopita na kupitisha azimio la kumkodisha Manji timu ya Yanga pamoja na nembo kwa miaka 10, Manji alisema Mwesigwa ambaye ni Katibu Mkuu wa sasa wa TFF si mzalendo na amekuwa akihujumu timu hiyo na ndio maana amewaburuza mahakamani.
Manji alisema iwapo wanachama hao wangekuwa na mapenzi na klabu hiyo, wasingeishtaki Yanga mahakamani, badala yake wangekuwa wavumilivu. Hata hivyo, Mwesigwa alishaweka wazi msimamo wake kuwa atahakikisha anapigania haki yake mpaka tone la mwisho na kuhakikisha anapata kile anachostahili.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba