KAMPUNI ya Acacia inayomiliki Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wilayani
hapa mkoani Shinyanga, imekabidhi hundi ya Sh milioni 717.2 kwa
Halmashauri ya Mji wa Kahama ikiwa ni ushuru wa huduma kwa kipindi cha
miezi sita iliyopita.
Akikabidhi hundi hiyo mbele ya wananchi wa Mji wa Kahama katika
viwanja vya Halmashauri ya Mji huo, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Assa
Mwaipopo, alisema kuwa ushuru huo wa huduma unapaswa kulipwa mara mbili
kwa mwaka.
Mwaipopo alisema kuwa fedha hizo zilizotolewa na mgodi huo ni
asilimia 0.3 ya faida wanayoipata katika uchimbaji madini hayo na
kuongeza kuwa ni za kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.
Alisisitiza kuwa kampuni yake itaendelea kuchangia ushuru huo kwa mujibu
wa sheria.
Aidha, alisema bila ya kuwa na uhusiano mzuri na Halmashauri ya Mji
wa Kahama na watu wake, kusingeweza kuwa na mafanikio makubwa baina ya
pande hizo mbili katika masuala mbalimbali ya kuchangia shughuli za
maendeleo katika jamii inayozunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Abel
Shija akipokea hundi hiyo alisema kuwa fedha hizo walizozipa zitatumika
kujenga hospitali ya rufaa katika mji huo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba aliwataka wawekezaji
hao kuhakikisha wanazifuatilia kampuni ndogo zilizopo katika mgodi huo
ili ziweze kulipa ushuru wa huduma kwa halmashauri hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu aliyekuwa mgeni
rasmi katika makabidhiano hayo, alisema mgodi huo hauna budi kuendelea
kuwa na uhusiano mzuri na wananchi wanaouzunguka mgodi huo kwa sababu
kufanya hivyo kutaibua fursa nyingi za maendeleo.
0 comments:
Post a Comment