MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa kufutwa kwa shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake na kuamuru kesi hiyo iendelee katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji Edson Mkasimongwa alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali hoja za rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kuamuru kesi hiyo iendelee pale ilipoishia kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo.
Katika rufaa hiyo, DPP alipinga uamuzi wa kufutwa kwa shitaka hilo uliotolewa na Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai kuwa alikosea kusema hati ya mashitaka ina dosari.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkasimongwa alisema amekubali kuwa kila kipengele katika Kifungu cha 12 cha Sheria ya Utakatishaji Fedha kinajitegemea kujenga kosa la utakatishaji fedha.
Aidha, alisema kutokana na hilo Hakimu Mchauru alikosea kusema hati ya mashitaka ina dosari na hata kama ilikuwa na dosari Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kuamuru shitaka hilo lifanyiwe marekebisho.
Jaji Mkasimongwa alisema, Kifungu cha 129 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinaeleza utaratibu unaotakiwa kufuatwa pale inapoona shitaka lina dosari na kufafanua kuwa shitaka linakuwa na dosari zinazohitaji ushahidi kuthibitisha na jingine ni la kwenye muundo wa hati ya mashitaka ambayo haihitaji ushahidi.
Alisema katika kesi hiyo dosari ipo kwenye muundo wa hati ambayo haihitaji ushahidi, hivyo Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kuamuru hati ya mashitaka ifanyiwe marekebisho.
Aidha, alisema Hakimu aliamua kufuta shitaka bila kueleza kwa nini hakutumia mamlaka yake kuamuru hati ifanyiwe marekebisho, hivyo alikosea kutoa uamuzi huo.
Katika kesi hiyo, Kitilya na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha ambalo lilihusisha Dola za Marekani milioni sita.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.
Hata hivyo, Aprili 27, mwaka huu, Mahakama ya Kisutu iliwafutia washtakiwa shitaka hilo baada ya upande wa utetezi kuiomba Mahakama iliondoe shitaka hilo kwa madai lina mapungufu ya kisheria, pia hakuna maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.
DPP alikata rufaa kupinga uamuzi huo hata hivyo Mahakama Kuu iliamuru kesi hiyo iendelee, lakini DPP alikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi huo na mahakama hiyo ikaamuru rufaa hiyo isikilizwe mbele ya jaji mwingine wa Mahakama Kuu.
0 comments:
Post a Comment