Tuesday, 9 August 2016

Wakuu wa nchi za EAC waombwa kusimamia amani, utulivu

WAKUU wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC), wameombwa kusimamia amani na utulivu wa kisiasa katika nchi za ukanda huo, kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kufanya shughuli zake bila matatizo.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Felix Mosha, alipozungumza na wanahabari, baada ya kumalizika kwa kikao cha Bodi ya baraza hilo jijini hapa.
Mosha aliwaomba wakuu wa nchi hizo ikiwemo Sudan Kusini kuhakikisha wanasimamia suala la utulivu wa kisiasa katika nchi zao ili kusaidia wafanyabiashara walioko katika nchi hizo kufanya biashara zao katika mazingira rafiki.
Alisema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina changamoto tofauti na kwamba kila nchi ni lazima ihakikishe inaweka mazingira mazuri ili watu wake wafanye biashara katika mazingira salama yasiyo na migogoro.
“Nchi za EAC zina matatizo tofauti hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunapambana kuhakikisha tunatatua changamoto hizo,” alisema Mosha.
Awali akifungua kikao cha Bodi hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Liberat Mfumukeko, aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha wafanyabiashara walioko katika sekta binafsi ndani ya jumuiya hiyo wanapiga hatua.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao hicho walisema kwa nyakati tofauti kuwa nchi wanachama katika baraza hilo zinapaswa kuwa na sera nzuri zinazoendana kwa lengo la kuziunganisha sekta binafsi kufanya biashara katika mazingira salama.
Kakee Dharwal ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza kutoka Tanzania, alisema suala la utungaji sera katika kila nchi wanachama wa baraza hilo, zinapaswa kuwa na sera zinazofanana kwa lengo la kuzisaidia sekta binafsi kufanya biashara.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba