Friday 12 August 2016

Magufuli ‘azika’ demokrasia

JOHN Magufuli, Rais wa Tanzania, ameonesha wazi dhamira ya kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa nchini katika kipindi cha utawala wake wa miaka mitano, anaandika Moses Mseti.
Julai 26 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilitangaza kufanya mikutano ya hadhara nchini chini ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.
Chadema kilitangaza Oparesheni ya Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) kwa kile walichodai kuwa, demokrasia nchini katika kipindi hiki cha miezi tisa ya Rais Magufuli inaminywa.
Rais Magufuli akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Furahisha Kata ya Kirumba Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, amesema hakuna kufanya siasa ‘uchwara’ na kwamba, ni muda wa kazi.
Amesema kuwa, kuna baadhi ya vyama vya siasa nchini kazi yao ni kutaka kufanya mikutano na maandamano na wakati kuwa muda wa kufanya siasa ulikwisha, muda huu ni wa kazi pekee hivyo na Watanzania wanapaswa kufanya kazi.
“Kufanya kazi ya kupata na kujenga barabara, viwanda na huduma ya afya hiyo ndio demokrasia pamoja na kupatikana kwa meli ziwa Victoria hiyo ndio demokrasia ya kweli hakuna demokrasia tofauti na hiyo,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa, watu wanaodai kwamba demokrasia imeminywa wakisahau kwamba, demokrasia ni kufanya kazi na bila kazi hiyo sio demokrasia ya kweli.
Pia rais amesisitiza kuwa kila mmoja anapasa kufanya siasa sehemu alikochaguliwa na kwamba kufanya hivyo kutasaidia uchumi wa taifa kukuwa na watu kupata maendeleo, kitendo ambacho kinapingwa na vyama vya siasa nchini.
Share:

Serikali: Hatuna ushahidi wa kuzihukumu shule za Feza

SERIKALI imesema haina ushahidi wa kutosha kuzitia hatiani shule za Feza nchini zinazodaiwa kumilikiwa na mmoja wa wananchi wa Uturuki anayetuhumiwa kujihusisha na ugaidi na kuitaka Serikali ya Uturuki kuwasilisha taarifa zenye ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma hizo.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga.
Alisema walipokea madai kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini kuwa shule hizo zinamilikiwa na mmoja wa wananchi wa nchi hiyo anayejihusisha na ugaidi.
Balozi Mahiga alisema katika madai ya ubalozi huo, shule hizo ni miongoni mwa miradi inayomilikiwa na mtuhumiwa huyo na kwamba, baadhi ya walimu wake hutumia mbinu za kigaidi kufundisha wanafunzi.
Akijibu tuhuma hizo, Balozi Mahiga alisema serikali kabla ya kutoa kibali kwa mwekezaji au mfanyabiashara yeyote kuendesha shughuli zake nchini, vyombo vya usalama nchini, hufanya upelelezi wa kina na wamejiridhisha kwamba wafanyabiashara wa Uturuki waliopo nchini wanafanya biashara halali.
“Ni kweli tumepokea tuhuma kutoka kwa Ubalozi wa Uturuki nchini kuhusu shule za Feza kwamba ni sehemu ya makundi ya kigaidi, lakini hatuwezi kuzitia hatiani shule hizo hadi tuletewe ushahidi wa kutosha,” alisema Balozi Mahiga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Feza, Habib Miradji alisema shule hizo ni za asasi iliyosajiliwa kisheria na Serikali ya Tanzania hivyo ni mali ya Tanzania na endapo kuna kitu au tatizo ni lazima wawasiliane na serikali na watafika kukagua ili kama kuna lolote baya hatua zichukuliwe.


Aidha alisema kwamba shule hazijafungwa.
Share:

Korti Kuu yarejesha shitaka alilofutiwa Kitilya

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa kufutwa kwa shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake na kuamuru kesi hiyo iendelee katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji Edson Mkasimongwa alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali hoja za rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kuamuru kesi hiyo iendelee pale ilipoishia kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo.
Katika rufaa hiyo, DPP alipinga uamuzi wa kufutwa kwa shitaka hilo uliotolewa na Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai kuwa alikosea kusema hati ya mashitaka ina dosari.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkasimongwa alisema amekubali kuwa kila kipengele katika Kifungu cha 12 cha Sheria ya Utakatishaji Fedha kinajitegemea kujenga kosa la utakatishaji fedha.
Aidha, alisema kutokana na hilo Hakimu Mchauru alikosea kusema hati ya mashitaka ina dosari na hata kama ilikuwa na dosari Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kuamuru shitaka hilo lifanyiwe marekebisho.
Jaji Mkasimongwa alisema, Kifungu cha 129 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinaeleza utaratibu unaotakiwa kufuatwa pale inapoona shitaka lina dosari na kufafanua kuwa shitaka linakuwa na dosari zinazohitaji ushahidi kuthibitisha na jingine ni la kwenye muundo wa hati ya mashitaka ambayo haihitaji ushahidi.
Alisema katika kesi hiyo dosari ipo kwenye muundo wa hati ambayo haihitaji ushahidi, hivyo Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kuamuru hati ya mashitaka ifanyiwe marekebisho.
Aidha, alisema Hakimu aliamua kufuta shitaka bila kueleza kwa nini hakutumia mamlaka yake kuamuru hati ifanyiwe marekebisho, hivyo alikosea kutoa uamuzi huo.
Katika kesi hiyo, Kitilya na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha ambalo lilihusisha Dola za Marekani milioni sita.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.
Hata hivyo, Aprili 27, mwaka huu, Mahakama ya Kisutu iliwafutia washtakiwa shitaka hilo baada ya upande wa utetezi kuiomba Mahakama iliondoe shitaka hilo kwa madai lina mapungufu ya kisheria, pia hakuna maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.
DPP alikata rufaa kupinga uamuzi huo hata hivyo Mahakama Kuu iliamuru kesi hiyo iendelee, lakini DPP alikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi huo na mahakama hiyo ikaamuru rufaa hiyo isikilizwe mbele ya jaji mwingine wa Mahakama Kuu.
Share:

Tanesco, TIB waamriwa kulipa fidia wananchi

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na benki ya TIB kuhakikisha wanalipa sehemu ya fidia iliyobaki ya Sh bilioni 46 kwa wananchi watakaopitiwa na mradi wa usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Somanga Fungu, Kilwa mkoani Lindi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.
Agizo hilo la Dk Kalemani limeelezwa linapaswa kuanza kutekelezwa kuanzia Agosti 17, mwaka huu.
Alitoa agizo hilo jana wakati wa kikao chake na wawakilishi wa wananchi watakaopitiwa na mradi huo, watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Tanesco na benki ya TIB.
Kikao hicho kililenga kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa fidia hiyo pamoja na kuunda kamati itakayofuatilia utekelezaji wa malipo kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Tanesco, hiyo ni baada ya kuonekana kuwa ulipaji wa malipo hayo ulikuwa ukisuasua na hivyo wananchi kuilalamikia serikali.
Alisema jumla ya fedha zinazopaswa kulipwa kwa wananchi hao katika wilaya za Temeke, Mkuranga, Kilwa, Ilala na Kinondoni ni Sh bilioni 79.
Share:

Wednesday 10 August 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUONGEZWA KWA MUDA WA KUFANYA MAOMBI KATIKA KOZI ZA CHETI NA DIPLOMA KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017

Baraza linapenda kuwaarifu wote walioomba kudahiliwa katika kozi za cheti na diploma na umma kwa ujumla kuwa muda wa nyongeza wa kutuma maombi kwa mwaka 2016/2017 umeongezwa hadi tarehe 13 Agosti 2016 ili kuruhusu ambao hawakukamilisha maombi yao kuyamaliza na ambao hawajafanikiwa kuomba kutuma maombi yao.

Baraza linaomba ifahamike kuwa vyuo na kozi zilizojaa hazitaonekana tena wakati wa maombi bali kozi zitakazoonekana ni zile zenye nafasi tu pia baraza linashauri waombaji wajipime na kuangali ushindani wa kozi ili kufanikisha kuchaguliwa kwao. Vyuo na kozi zilizo na nafasi zimeainishwa hapa.

Baraza pia linapenda kuwaarifu waombaji waliofanya maombi kwenye vyuo vya Ualimu vya Serikali kuwa uteuzi kwenye vyuo hivyo unasubiri mwongozo wa Serikali na hivyo watafahamishwa punde uteuzi utakapokamilika. Waombaji wa vyuo hivi wanashauriwa kusubiri na kutokubadili machaguo yao hadi kutangazwa kwa uteuzi kwa vyuo vya Ualimu vya Serikali.

Baraza pia linapenda kuwataarifu waombaji waliokwisha chaguliwa kwenye awamu ya kwanza na wanataka kuomba uhamisho kutoka kozi ama chuo kimoja kwenda kingine wavute subira utaratibu utatolewa mara tu majibu ya waombaji wa awamu ya pili yatakapotolewa.

Aidha Baraza linapenda kuwafahamisha waombaji wa Shahada ya Kwanza (Bachelor Degree) waliofanya maombi kupitia mfumo wa pamoja wa udahili wa Baraza kuwa utaratibu wa kukamilisha maombi yao utatolewa baada ya mashauriano kati ya Baraza na Tume ya Vyuo Vikuu yatakapokamilika.

Imetolewa na
Ofisi ya Katibu Mtendaji
NACTE
Tarehe: 08th Agosti, 2016
Share:

Bilionea wa milioni 7/- kwa dakika akwama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya kufutwa kwa shitaka la utakatishaji fedha katika katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 14 inayomkabili, mfanyabiashara Mohammed Yusufali ‘Choma’ na mwenzake.
Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo. Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa wataendelea kusota rumande hadi kesi itakapokwisha kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana.
Katika kesi hiyo Choma aliyewahi kutajwa kujipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali, pamoja na mfanyabiashara Samuel Lema, wanakabiliwa na mashitaka 222 ya kula njama, kutakatisha fedha, na kuisababishia serikali hasara hiyo kwa kukwepa kulipa kodi.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema Mahakama imetupilia mbali maombi hayo yaliwasilishwa na upande wa utetezi kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Alisema mahakama inakubali kuwa hati ya mashitaka inayowahusu washitakiwa hao haina makosa, hivyo Mahakama haiwezi kubadili hati hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Aidha aliongeza kuwa, kama upande wa utetezi ungekuwa na nia ya kutaka kufutwa kwa shitaka hilo ungewasilisha maombi hayo tangu awali. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Katika hoja za ombi hilo, Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa aliomba shitaka hilo kufutwa kwa kuwa lina mapungufu kisheria na kuongeza kuwa si kila kosa la wizi na kughushi ni utakatishaji fedha, bali makosa yanayofuata baada ya vitendo hivyo yaani kuficha chanzo au asili ya upatikanaji wa fedha hizo ndiyo kosa la utakatishaji.
Alidai maelezo ya kwenye shitaka la 221 hayajengi kosa la utakatishaji fedha hivyo aliiomba mahakama ifute shitaka hilo ili waendelee na mashitaka mengine.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa halina msingi kisheria na shitaka hilo lina maelezo ya kutosha kujenga kosa la utakatishaji wa fedha.
Share:

Tuesday 9 August 2016

Tanzania yaanza vibaya Olimpiki

TANZANIA jana ilianza vibaya Michezo ya 31 ya Olimpiki baada ya mchezaji wake wa judo, Andrew Thomas Mlugu kudundwa na Jake Bensted wa Austria katika mchezo wa kilo 73.
Tanzania katika michezo hiyo iliyoanza Agosti 5, imepeleka wachezaji saba, judo akiwa mchezaji mmoja, wawili wa kuogelea, ambao ni Magdalena Moshi na Hilal Hilal na wale wa riadha, ambao bado hawajaenda Rio kutokana na ratiba yao kuwa mwishoni.
Mchezaji huyo wa judo alishiriki mashindano hayo kupitia tiketi ya upendeleo baada ya kushindwa kufuzu kwa njia ya kawaida.
Share:

Manji kutinga kizimbani leo

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji leo atapanda kizimbani Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi alikoburuzwa na waliokuwa watendaji wa klabu hiyo, Selestine Mwesigwa na Luis Sendeu.
Septemba mwaka 2012, Mwesigwa akiwa Katibu Mkuu wa Yanga na Sendeu akiwa Ofisa Habari wa klabu hiyo ya Jangwani, waliondolewa katika ajira zao kwa kile kilichoelezwa kuwa utendaji mbovu.
Mwesigwa na Sendeu waliomba bila mafanikio walipwe na Yanga fidia ya Sh 262 milioni, ambapo kati ya hizo, Sendeu anadai Sh 79 milioni na Mwesigwa anadai Sh 183 milioni.
Watendaji hao walifikisha suala hilo katika Baraza la Kazi ambapo walishinda madai yao na hivyo Yanga iliamriwa kuwalipa kiasi hicho cha fedha hata hivyo fedha hizo bado hawajalipwa kitendo ambacho kimeilazimu Mahakama kumuita kwa nguvu Mwenyekti huyo wa Yanga leo bila kukosa.
Wito huo ulitolewa Juni 24, ambapo Manji ametakiwa kufika mahakamani leo Agosti 9 saa 3:00 asubuhi bila kukosa wala kutuma mwakilishi.
“Unatakiwa kufika binafsi mbele ya Mahakama hii ikikaa Dsm tarehe 9, mwezi wa nane mwaka 2016 mbele ya Mheshimiwa Ujimo na kubaki Mahakamani hadi uruhusiwe na Mahakama kuondoka kwa ajili ya kutajwa, kusikilizwa kwa marejeo/ maombi/mgogoro na unatakiwa kujibu hati ya kiapo ndani ya siku 15."
Katika kikao cha dharura cha klabu hiyo kilichokaa Jumamosi iliyopita na kupitisha azimio la kumkodisha Manji timu ya Yanga pamoja na nembo kwa miaka 10, Manji alisema Mwesigwa ambaye ni Katibu Mkuu wa sasa wa TFF si mzalendo na amekuwa akihujumu timu hiyo na ndio maana amewaburuza mahakamani.
Manji alisema iwapo wanachama hao wangekuwa na mapenzi na klabu hiyo, wasingeishtaki Yanga mahakamani, badala yake wangekuwa wavumilivu. Hata hivyo, Mwesigwa alishaweka wazi msimamo wake kuwa atahakikisha anapigania haki yake mpaka tone la mwisho na kuhakikisha anapata kile anachostahili.
Share:

Simba yaleta raha

SIMBA jana ilisherehekea vizuri miaka 80 tangu ilipoanzishwa baada ya kuichabanga AFC Leopards ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa tamasha la `Simba Day’ kwenye Uwanja wa Taifa.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog juzi aliwataka wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa kushuhudia kikosi kitakachotwaa taji la Tanzania Bara msimu wa mwaka 2016/2017.
Simba ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 38 lililowekwa kimiani na Ibrahim Ajibu baada ya kupiga shuti kali la moja kwa moja akipokea pasi ya Mussa Ndusha.
Mchezaji hodari Laudit Mavugo alidhihirisha makali yake pale aliposaidia kupatikana kwa bao la pili lililofungwa tena na Ajib baada ya kumtengenezea mpira safi alioujaza wavuni katika dakika ya 57.
Shiza Kichuya aliyejiunga akitokea Mtibwa, aliiandikia Simba bao la tatu katika dakika ya 66 akimalizia kazi nzuri ya Ajibu na Mavugo, ambao waligongeana vizuri kabla mpira haujamkuta mfungaji aliyeujaza wavuni. Wekundu hao wa Msimbazi waliandika bao la nne lililofungwa na Mavugo baada ya kufanya kazi nzuri uwanjani.
Simba awali walikosa mabao mengi na hii ilitokana na kutoelewana kwa Frederic Blagnon na Kichuya. Wenyeji Simba walifanya shambulizi la nguvu katika dakika ya 28 na kupata kona kupitia kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, kona hiyo haikuzaa matunda. Awali, Ajibu nusura aigharimu timu yake baada ya kumchezea rafu Jack Kiyai wa AFC Leopards na kupatiwa kadi ya njano katika dakika ya 35 na kuamuriwa upigwe mpira wa adhabu, ambao haukuzaa matunda.
Safu ya kiungo ya Simba imeonekana kuimarika zaidi ikiongozwa na Jonas Mkude, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hiyo ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Katika kuadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwa klabu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Hamisi Kingwangalla, Profesa Athumani Kapuya, Mohamed Dewji `Mo’, pamoja na viongozi wa Simba, walikata keki wakati wa mapumziko.
Simba: Vicent Agban, Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Janyie Buifunga, Novaty Lufunga, Method Mwanjale, Mwinyi Kazimoto, Mussa Ndusha, Frederic Blagnen, Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya.
Share:

Brazil kuwekeza kwenye umeme nchini

SERIKALI ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Balozi wa Brazil nchini, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo naye. Balozi Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake ina ujuzi na uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali hususan maji.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya viwanda, unahitaji umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.
Alitaja eneo lingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa chanzo kizuri cha nishati safi.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo ambayo Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa kuwekeza Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na Serikali.
Alisema, kunaandaliwa utaratibu maalumu utakaokuwa wa wazi na kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya kupunguza au kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu unaotumika katika majadiliano pasipo sababu za msingi.
Share:

Mafisadi fedha za miradi kukiona

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Tano, itapambana kwa nguvu zote na vitendo vya ufisadi kwenye fedha, zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, kudhibiti matumizi yasiyo lazima na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi ili fedha zinazokusanywa, zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.
Alisema hayo jana wakati akifunga maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima ya Nanenane kitaifa katika Uwanja wa Ngongo mkoani Lindi kwa niaba ya Rais John Magufuli.
Katika hotuba yake kwa mamia ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, Makamu wa Rais alisema azma ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo itatimia, iwapo tu vitendo vya ufisadi katika fedha zinazoelekezwa kwenye maendeleo utakoma.
Alisema pia hayo yatawezekana endapo wananchi wataunga mkono jitihada za serikali katika kulipa kodi kwa wakati, kudai risiti, kufanya kazi kwa bidii na kukemea vitendo vya rushwa kama hatua ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tuna dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia na kuwaboreshea huduma zote za kijamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla bila kujali mikoa mnayotoka, jinsia, dini au itikadi za vyama vyenu.”
Kuhusu uimarishaji wa shughuli za kilimo nchini, Samia alisema maadhimisho ya Nanenane ni moja ya juhudi za serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi katika taifa, ambapo asilimia 75 ya wananchi wanajihusisha na shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi kote nchini.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuzipa kipaumbele sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na kuongeza bajeti katika sekta hizo ili ziweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Aliwaeleza wananchi kuwa serikali imeweka mikakati na mipango inayolenga kusaidia uimarishaji wa shughuli za kilimo kote nchini kwa kuongeza matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491 mwaka 2005/2006 hadi 16,478 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hivyo kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 12.
Alifafanua kuwa serikali imeongeza idadi ya maofisa ugani katika kilimo kutoka 3,379 mwaka 2005 hadi 2006 hadi 8,756 mwaka 2015/2016 na serikali pia imefufua mashamba ya mbegu kwa kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kuzalisha mbegu bora za mazao ya chakula nchini.
Matarajio ya wananchi
Akizungumzia matarajio ya wananchi, Samia alisema serikali inajua wananchi wana matarajio makubwa ya uongozi wao hivyo itahakikisha inaboresha huduma na uchumi wa Watanzania wote.
“ Tunajua mna matarajio makubwa na uongozi wa awamu ya tano, basi niwaahidi kuwa serikali yenu itahakikisha inaimarisha huduma na uchumi kwa usawa bila kuwa na upendeleo wa mikoa mnayotoka, itikadi ya dini na siasa,” alisema.
Aidha alisema ni vyema uongozi wa mikoa hiyo kuhakikisha wanaendeleza mashamba katika mikoa yao wayatumie kuwaelimisha wananchi njia bora za kilimo. Pia aliwataka wananchi kusaidia juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa kulipa kodi, kupambana na rushwa na wafanyakazi wazembe na wavivu.
“Ningependa kuwaomba wananchi kuiunga mkono mikakati ya serikali ambayo ina lengo la kuwaletea mabadiliko chanya. Watanzania wote mnatakiwa kulipa kodi kama inavyotakiwa ili kufanikisha malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2020, alisema.
Kwa upande wa ufugaji, Samia alisema serikali inaboresha wataalamu wa mifugo ambapo wenye elimu ya Diploma wameongezeka kutoka 2,451 mwaka 2015 hadi 2,500 mwaka huu, wakati wale wenye Cheti wameongezeka kutoka 1,034 mwaka 2015 hadi 1,466 mwaka 2016 huku 1,471 wakihitimu Shahada mwezi Juni mwaka huu.
Alisema mpaka Juni mwaka huu kulikuwa na upungufu wa wataalamu 8,725 nchi nzima.
Kwa upande wa uvuvi, Samia alisema idadi ya mabwawa imeongezeka kutoka 21,300 mwaka 2014/2015 hadi 22,500 mwaka 2015/2016.
Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha ifikapo 2020, ajira kwa vijana inaongezeka hadi kufikia asilimia 40 na kuwataka vijana kuchangamkia fursa za ajira zinazojitokeza.
Atembelea banda la TSN
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliipongeza Kampuni ya magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers Limited (TSN) kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kupitia magazeti yake, likiwamo gazeti mtandao.
TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili, SpotiLeo na gazeti mtandao linalopatikana kwa anwani ya www. dailynews.co.tz na www.habarileo. co.tz.
Alitoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la TSN kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini katika viwanja vya Ngongo mjini Lindi. Pia alivutiwa jinsi TSN inavyoendesha gazeti mtandao na kuahidi kuwa atajiunga na huduma ya gazeti mtandao haraka iwezekanavyo.
“Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya nami nitajiunga na magazeti mtandao ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo,” alisema huku akitaka kujua kama huduma hiyo ni ile ya kupata ukurasa wa mbele na nyuma pekee.
Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa TSN, Prosper Mallya alimwambia Makamu wa Rais kuwa magazeti mtandao yana kurasa zote kama ilivyo kwa magazeti ya kawaida, lakini yanauzwa kwa nusu bei.
“Daily News mtandao inauzwa kwa Sh 500, HabariLeo kwa Sh 400 na SpotiLeo inauzwa kwa Sh 250, bei ambazo ni nusu ya bei za magazeti ya kawaida,” alisema.
Mratibu wa Toleo Maalumu katika Magazeti ya TSN, Dativa Minja alimwambia Makamu wa Rais kuwa TSN imekuwa ikiandika habari, makala mbalimbali na uchambuzi katika masuala ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kuwa wakulima wananufaika kwa kusoma magazeti hayo.
Share:

Wakuu wa nchi za EAC waombwa kusimamia amani, utulivu

WAKUU wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC), wameombwa kusimamia amani na utulivu wa kisiasa katika nchi za ukanda huo, kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kufanya shughuli zake bila matatizo.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Felix Mosha, alipozungumza na wanahabari, baada ya kumalizika kwa kikao cha Bodi ya baraza hilo jijini hapa.
Mosha aliwaomba wakuu wa nchi hizo ikiwemo Sudan Kusini kuhakikisha wanasimamia suala la utulivu wa kisiasa katika nchi zao ili kusaidia wafanyabiashara walioko katika nchi hizo kufanya biashara zao katika mazingira rafiki.
Alisema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina changamoto tofauti na kwamba kila nchi ni lazima ihakikishe inaweka mazingira mazuri ili watu wake wafanye biashara katika mazingira salama yasiyo na migogoro.
“Nchi za EAC zina matatizo tofauti hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunapambana kuhakikisha tunatatua changamoto hizo,” alisema Mosha.
Awali akifungua kikao cha Bodi hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Liberat Mfumukeko, aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha wafanyabiashara walioko katika sekta binafsi ndani ya jumuiya hiyo wanapiga hatua.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao hicho walisema kwa nyakati tofauti kuwa nchi wanachama katika baraza hilo zinapaswa kuwa na sera nzuri zinazoendana kwa lengo la kuziunganisha sekta binafsi kufanya biashara katika mazingira salama.
Kakee Dharwal ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza kutoka Tanzania, alisema suala la utungaji sera katika kila nchi wanachama wa baraza hilo, zinapaswa kuwa na sera zinazofanana kwa lengo la kuzisaidia sekta binafsi kufanya biashara.
Share:

Acacia yatoa ushuru wa huduma wa mil 717.2/-

KAMPUNI ya Acacia inayomiliki Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wilayani hapa mkoani Shinyanga, imekabidhi hundi ya Sh milioni 717.2 kwa Halmashauri ya Mji wa Kahama ikiwa ni ushuru wa huduma kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.
Akikabidhi hundi hiyo mbele ya wananchi wa Mji wa Kahama katika viwanja vya Halmashauri ya Mji huo, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Assa Mwaipopo, alisema kuwa ushuru huo wa huduma unapaswa kulipwa mara mbili kwa mwaka.
Mwaipopo alisema kuwa fedha hizo zilizotolewa na mgodi huo ni asilimia 0.3 ya faida wanayoipata katika uchimbaji madini hayo na kuongeza kuwa ni za kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu. Alisisitiza kuwa kampuni yake itaendelea kuchangia ushuru huo kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema bila ya kuwa na uhusiano mzuri na Halmashauri ya Mji wa Kahama na watu wake, kusingeweza kuwa na mafanikio makubwa baina ya pande hizo mbili katika masuala mbalimbali ya kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii inayozunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Abel Shija akipokea hundi hiyo alisema kuwa fedha hizo walizozipa zitatumika kujenga hospitali ya rufaa katika mji huo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba aliwataka wawekezaji hao kuhakikisha wanazifuatilia kampuni ndogo zilizopo katika mgodi huo ili ziweze kulipa ushuru wa huduma kwa halmashauri hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu aliyekuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo, alisema mgodi huo hauna budi kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na wananchi wanaouzunguka mgodi huo kwa sababu kufanya hivyo kutaibua fursa nyingi za maendeleo.
Share:

Familia 8 zanusurika kufa kwa moto

FAMILIA nane zenye watu zaidi ya 20 kwenye mtaa wa Mharakani kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani zimenusurika kufa baada ya moto kutokea wakati wanafamilia hao wakiwa wamelala.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, waathirika wa tukio hilo la moto walisema lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 8, mwaka huu saa 6:30 usiku.
Mmoja wa waathirika hao, Emmanuel Mhina, alisema watu waliokuwa jirani na nyumba yao ndio waliowafahamisha juu ya moto huo ambao unasadikiwa ulianzia kwenye moja ya maduka yaliyo kwenye nyumba hiyo.
Alisema kuwa walikuwa wamelala lakini ilipofika saa saba kasorobo usiku, waliamshwa na watu na walipoamka walikutana na moto mkubwa ambao hawakujua ulianza saa ngapi ndipo walipoanza kujiokoa.
“Tunamshukuru Mungu tumenusurika licha ya mali zetu zote kuteketea kwa moto ambao ulianzia kwenye moja ya maduka ambayo yameungana,” alisema Mhina.
Naye Said Juma alisema kuwa moto huo umewapa hasara kubwa kwani amepoteza vitu karibu vyote na kufanikiwa kuokoa vichache hali ambayo inamfanya aanze upya maisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Yahaya Abdalah, alisema kuwa wananchi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Jeshi la Polisi walifanikisha kuzimwa kwa moto huo.
Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege, Robert Machumbe, alisema kuwa waathirika hao hawakuweza kuokoa kitu kwani vitu vyote viliteketea kwa moto huo.
Katika hatua nyingine, mtoto mwenye umri kati ya miaka minne na nusu amenusurika kufa katika moto huo baada ya mama yake kumwacha kwenye nyumba hiyo akiwa amemfungia na kwenda kusikojulikana.
Inaelezwa kuwa, mtoto huyo aliokolewa na mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye ni miongoni mwa waliounguliwa na nyumba hiyo baada ya kujitosa kumwokoa.
Share:

Uteuzi alioufanya Waziri Nape leo August 09 2016



Kufuatia uhamisho wa aliyekuwa mkurugenzi wa Idara ya habari-Maelezo Assah Mwambene uliofanyika March 7 2016 kwenda wizara ya mambo ya nje ushirikiano wa kikanda na kimataifa ulianza mchakato wa kumpata mkurugenzi mwingine.
Leo August 9 2016 Waziri wa Habari, Utamaduni sanaa na michezo, Nape Nnauye amemteua Mkurugenzi wa idara ya Habari-Maelezo Hassan Abbas kuziba nafasi ikiyoachwa wazi na Assah Mwambene Kabla ya uteuzi huo Hassan Abbas alikuwa ni meneja Habari na Mawasiliano katika ofisi ya Rais inayosimamia utekelezaji wa program ya matokeo makubwa sasa.
Share:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba