Thursday, 1 September 2016

WATUMISHI 15 SIHA WAHOJIWA IKULU

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Valerian Jual, amesema watumishi 15 wa halmashauri hiyo wanaohojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokana na tuhuma mbalimbali.
Jual alitoa taarifa hizo juzi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadik, aliyetembelea wilaya ya Siha kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Alisema licha ya watuhumiwa hao, pia watumishi wengine watano walishikiliwa na jeshi la Polisi kwa kukosa dhamana wakituhumiwa kusafirisha jenereta tano zilizotumika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na vifaa vya pikipiki kwenda kusikojulikana.
Jual alisema, hadi sasa taasisi za serikali zinaendelea na uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao, kwa lengo la kumaliza uozo na ubadhirifu mali za serikali ambapo uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Tuhuma zinazowakabili watumishi hao (majina yamehifadhiwa), ni pamoja na kushindwa kuthibitisha uhalali wa malipo zaidi ya Sh milioni 70 ambazo ni fedha za uhamisho wa walimu, motisha, utengenezaji wa madawati na uchaguzi, fedha za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zaidi ya Sh milioni 50 na fedha za uchomaji takataka za uchaguzi huo Sh milioni 10.
Mkurugenzi huyo pia alikanusha uvumi unaoenezwa kuwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha, ndilo lililoibua tuhuma hizo, ambapo ameeleza haikuwa ajenda ya bazara hilo, bali ilikuwa ni ajenda ya taasisi za serikali ya siku nyingi katika kusafisha halmashauri zote nchini ikiwamo ya Siha.
"Tangu nilipokabidhiwa ofisi, ndipo taasisi za serikali ziliingia ofisini kwangu kwa ajili ya kufanya uchunguzi na sio ajenda ya baraza la madiwani kama inavyodaiwa, katika uchunguzi huo nimepata ushirikiano mzuri sana katika taasisi za serikali hususani ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo," alisema Jual.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba