Thursday, 1 September 2016

NINA IMANI NA VIONGOZI WALIOCHAGULIWA KWA HAKI

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Rais wa Botswana, Dk Seretse Kahama Ian Khama, amempongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana.
Rais huyo wa Botswana alitoa pongezi hizo kupitia hotuba aliyoitoa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC unaofanyika Mbabane- Swaziland ambako Dk Magufuli anawakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Dk Khama alisema, ukuaji wa demokrasia katika nchi wanachama wa SADC unaendelea kuimarika hivyo ni muhimu jitihada hizo zikaendelezwa zaidi.
Amesema, ana imani na viongozi waliochaguliwa kwa njia ya amani, uhuru na haki katika ukanda wa SADC akiwemo Rais wa Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli kwamba watafanya kazi kwa bidii kuharakisha maendeleo kwa wananchi wao.
Viongozi wa nchi za SADC waliokuwa katika mkutano huo walishuhudia zawadi mbalimbali zikitolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye utunzi wa insha na kwa wanahabari walioandika habari mbalimbali kuhusu SADC, ikiwemo masuala ya huduma ya maji.
Aidha, katika mkutano huo wa 36 wa SADC, viongozi wanaohudhuria watafanya uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama ( SADC Troika).
Katika mkutano huo, wakuu wa nchi na Serikali watapokea rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali kutoka kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutia saini.
Miongoni mwa rasimu hizo ni mkataba wa kuboresha Itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya Itifaki ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC na maboresho ya Itifaki ya Biashara.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba