Monday, 5 September 2016

MAMIA WAUAGA MWILI WA MKURUGENZI WA MAREHEMU A TO Z

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameongoza wakazi wa mkoa huo kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha A to Z , Anuj Shah, cha jijini hapa, kinachotengeneza vyandarua vyenye dawa.
Mwili wa Shah uliagwa jana na wafanyakazi wa kiwanda hicho, majirani wa kiwanda hicho, pamoja na rafiki zake kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Uliagwa katika makazi yake yaliyopo Kisongo na baadaye kuzikwa kwa kuchomwa moto kwenye makaburi ya Esso jijini hapa.
Akizungumza wakati wa maziko, Gambo alisema Shah alipenda kila Mtanzania mwenye nguvu apate ajira, ili kuendesha maisha ya familia yake, ndio maana aliamua kuajiri Watanzania walioishia darasa la saba na kuwafundisha kazi mbalimbali za ufundi kiwandani hapo.
"Niseme tu kuwa kampuni imepoteza mtu muhimu. Shah alikuwa na mapenzi makubwa na Watanzania na alitaka kila mtu apate ajira wakiwemo wanawake na wanaume, walemavu na wasio na ulemavu. Alikuwa rafiki wa familia yangu pia," Gambo alisema.
Aliutaka uongozi wa A to Z kuenzi maono ya Shah kwa kuongeza ajira zaidi ili kupunguza idadi ya Watanzania wasio na ajira.
Shah ni miongomi mwa waliogundua chandarua chenye dawa hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watu kutokana na ugonjwa wa malaria, husan mama wajawazito na watoto wanaotumia zaidi vyandarua hivyo.
Gambo aliongeza kuwa, katika kuonesha mapenzi yake kwa Watanzania, mwaka jana kwa kushirikiana na watafiti mbalimbali kupitia kituo chake cha utafiti cha ATRC, Shah aligundua mifuko ya kuhifadhia mahindi kwa muda mrefu bila kutobolewa na wadudu ikiwemo dumuzi.
Ilielezwa kuwa Shah alifariki dunia Septemba mosi mchana katika Hospitali ya MP Shah ya Jijini Nairobi alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na shinikizo la damu.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba