Thursday, 1 September 2016

VITAMBULISHO VYA UTAIFA KUKOMESHA WAHAMIAJI HARAMU KIGOMA

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kabwe Zitto
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamelalamikia operesheni ya kukamata wahamiaji haramu inayoendelea mkoani Kigoma na kupendekeza kuwa ili kumaliza tatizo hilo, serikali haina budi kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mkoa huo.
Wakizungumza katika mkutano wa kujadili mpango wa Tushirikishane unaosimamiwa na Jamii Forum, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo, walisema kuwa ukamataji unaofanyika sasa, unakiuka haki za wananchi.
Diwani wa Kata ya Kigoma Mjini, Hussein Kalyango alisema, katika ukamataji huo ambao hufanywa na polisi wakati wa usiku, umekuwa ukinyanyasa raia kwani wakati mwingine wanaokamatwa huachiwa bila kupewa fidia yoyote baada ya kusota rumande kwa zaidi ya siku tatu na kufanyiwa unyanyasaji mwingine.
Diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini, Clayton Revocatus alisema, wameshalalamikia jambo hilo kwa uongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji mkoani Kigoma, lakini wamekuwa wakipata majibu ya vitisho na kukatisha tamaa, jambo linaloashiria kwamba unyanyasaji huo wa raia kwa tuhuma za uhamiaji haramu, hazitaisha katika siku za karibuni.
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kabwe Zitto alisema, suala la uhamiaji haramu kwa wananchi wa mkoa huo, ni tatizo kubwa na walishaanza kulishughulikia kwa kufanya vikao na watu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), lakini mabadiliko ya viongozi wa taasisi hiyo yamefanya jambo hilo kutotekelezwa kwa sasa.
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mkoa wa Kigoma inamshikilia Ofisa Uhamiaji wa Wilaya Uvinza, Novat Kato (46) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Raphael Mbwambo alisema, mtuhumiwa huyo alipokea Sh milioni 8.1 Novemba mwaka jana, kutoka kwa wakulima kutoka Burundi, waliokuwa wakilima na kuishi nchini bila vibali kwa lengo kuwapatia vibali vya kuishi na kufanya kazi kinyume cha taratibu za utendaji wa idara hiyo.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba