KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imesema ongezeko la mapato ya Sh bilioni 1.9 halina uhusiano wowote na ufungwaji wa mtambo mpya wa kuratibu mapato ya kampuni ya simu au kodi ambazo hazijalipwa kipindi cha nyuma, bali limetokana na Sheria mpya ya Kodi ya Mwaka 2016.
Aidha, imefafanua kuwa katika kipindi kifupi mabadiliko hayo yataongeza pato la serikali, lakini mabadiliko hayo yanaonesha kwamba matokeo hayo yatapunguza watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kutokana na watumiaji kutomudu gharama.
Kampuni hiyo ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao, sheria hiyo mpya imeongeza wigo wa kodi katika sekta ya mawasiliano kwa kuongeza asilimia 10 ya kodi ya zuio katika kutoa fedha kwenye simu na sio makato ya kufanya miamala.
Alisema kutokana na watumiaji wake wengi kutoweza kumudu gharama zake na mapato yalioongezeka yatapungua, hali ambayo itarudisha nyuma jitihada za pamoja za kuwezesha Watanzania kuwa kwenye mfumo rasmi wa matumizi ya fedha.
“…ongezeko ambalo ni mbali na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo inakuwa tayari imelipwa. Matokeo ya ongezeko hili malipo yetu ya kodi yameongezeka kufikia shilingi bilioni 1.6 kwa mwezi,” alisema Ferrao.
Alisema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia pato la serikali na kushiriki kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia nyanja mbalimbali. Pia kampuni hiyo inaongoza katika sekta ya mawasiliano kwa kukusanya na kulipa kodi ya mapato nchini Tanzania.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi 2016, Vodacom Tanzania ilichangia zaidi ya Sh bilioni 367 katika makusanyo ya kodi za serikali.
Sekta ya mawasiliano nchini Tanzania ni ya pili kwa kutozwa kodi kubwa katika bara zima la Afrika hali ambayo inazidisha changamoto kwa wawekezaji wa sekta hiyo hususani katika kujenga miundombinu bora.
Sheria mpya ya fedha ya mwaka huu iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato kutoka katika kampuni za simu.
0 comments:
Post a Comment