Monday, 5 September 2016

TRA YAFUNGA AKAUNTI ZA MSALABA MWEKUNDU

HALI imezidi kuwa tete ndani ya Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzifunga akaunti zaidi ya nne za chama hicho kutokana na kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi ya makato ya mshahara wa wafanyakazi (PAYE).
Taarifa kutoka ndani ya TRCS zinaeleza kuwa kodi inayodaiwa na TRA ni ile ya PAYE ya wafanyakazi zaidi 200 wanaofanya kazi mkoani Kigoma katika kambi za wakimbizi kati ya mwaka 2011/2015.
Kodi hiyo inakadiriwa kufikia shilingi milioni 790 huku chama hicho kikidaiwa pia shilingi bilioni 1.5 malimbikizo ya kodi ongezeko la thamani (VAT) na mapato kutokana mauzo ya magari.
Hali ndani ya TRCS imeelezwa kuwa mbaya kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kujitumbukiza katika vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa TRA imechukua uamuzi wa kufunga akaunti hizo baada ya kufanya mawasiliano ya muda mrefu na uongozi wa chama hicho ambao hata hivyo, ulishindwa kulipa malimbikizo ya kodi hizo.
Raia Mwema imebaini kuwa akaunti zilizofungwa zipo katika benki ya NBC Ltd tawi la Kigoma, benki ya CRDB tawi la Kigoma na nyingine iliyopo benki ya NMB tawi la Kasulu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa pia akaunti za chama hicho zilizopo katika benki mbili kubwa jijini Dar es Salaam zimefungwa ikiwa ni hatua zaidi za TRA kuibana chama hicho.
Taarifa za ndani zaidi kutoka TRCS na uthibitisho wa nyaraka mbalimbali zinaeleza kuwa fedha hizo za makato ya kodi ya PAYE zilitumiwa kifisadi na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Sakata hilo la TRCS kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi hiyo lilianza mwanzoni mwa mwaka huu hasa baada ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu tano ambayo imekuwa ikisisitiza na ikisimamia kwa weledi ulipaji wa kodi.
Mei 30 mwaka huu Kaimu Katibu Mkuu wa TRCS, Peter Mlebusi, alimwandikia Waziri Fedha, Dk. Philip Mpango, kwa barua yenye kumbukumbu namba TRCS/T/1/264  akimwomba waziri huyo kwa mamlaka yake kufuta deni la malimbikizo ya kodi hizo.
Hata hivyo maombi hayo ya TCRS yalijibiwa Juni 21 mwaka huu kwa barua yenye kumbukumbu namba CAB.481/547/01 kutoka Wizara Fedha kuwa hakuna mamlaka ya kisheria kwa chama hicho kusamehewa kulipa malimbikizo ya kodi hiyo.
Barua hiyo ambayo imesainiwa na Doto M. James kwa niaba ya Katibu wa Wizara hiyo, imebainisha kuwa TRCS ni lazima walipe kodi hiyo kama sheria inavyoelekeza kwa kuwa maombi yote ya kusamehewa  kodi kwa kawaida hupitishwa kwa tangazo katika gazeti la serikali (GN).
Pamoja na barua hiyo ya Wizara, TRCS waliendelea kung’ang’ania kutolipa kodi hiyo ambapo Kaimu Katibu Mkuu Mlebusi alimwandikia barua nyingine Kamishna Mkuu wa TRA, Julai 18 mwaka huu, kuwa chama hicho kisamehewa kulipa riba ya shilingi 279,543,521.74.
Kwa mujibu barua hiyo yenye kumbukumbu TRCS/T/1/267, Mlebusi anadai kuwa kodi wanayodaiwa ni shilingi 510,848,086.85  na chama hicho ni chama  hiari (charitable organization) hivyo hawatengenezi faida.
Kutokana na mvutano huo wa muda ndipo wiki iliyopita TRA walipofanya uamuzi wa kufunga akaunti za chama hicho hatua ambayo imetajwa kuathiri shughuli za chama hicho kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na Raia Mwema Jumanne wiki hii, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRCS aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema kufungwa kwa akaunti hizo kunahatarisha chama hicho kutimiza malengo yake.
 “Hali hii inatishia malengo ya chama ambayo ni kusaidia jamii pale inapopatwa na majanga ya kibinadamu yanayosababishwa na vita, maradhi au majanga ya asili,” alisema mjumbe huyo.
Mjumbe huyo aliongeza kuwa hatua hiyo pia imechafua taswira ya chama hicho mbele ya jamii ya kimataifa hivyo kuna uwezekano mkubwa wafadhili kusitisha misaada yao hatua ambayo itaathiri wananchi wanaokabiliwa na majanga mbalimbali ambao wanapata misaada kupitia TRCS.
"Mamlaka za serikali kama Takukuru na ofisi ya rais ambaye ndiye mlezi wa chama wanatakiwa kuchunguza haraka ufisadi wa viongozi wa juu na matumizi mabaya ya madaraka ili kuinusuru taasisi ambayo ni nyeti sana kwa maslahi ya nchi yetu," aliongeza
Share:

MAYANGA ATAMBIA KIKOSI CHAKE

KOCHA wa Mtibwa Sugar Salum Mayanga amesema ushindi walioupata katika mchezo dhidi ya Majimaji umetokana na juhudi za kuboresha kikosi chake mara kwa mara pindi wanapobaini mapungufu.
Mtibwa Sugar iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Majimaji,Songea.
Ushindi huo unaifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi sita baada ya kushinda michezo miwili dhidi ya Ndanda FC mabao 2-1 na Majimaji mabao 2-1 na kufungwa mmoja dhidi ya Ruvu Shooting.
Akizungumza na gazeti hili, Mayanga alisema kikosi chake kilifanikiwa kupata ushindi huo baada ya kutumia nafasi walizopata na kwamba wanategemea kuendelea na harakati zao za kupata matokeo ya ndani na nje ya uwanja wao.
“Tunashukuru kwa kupata pointi tatu ugenini, unajua tulivyopoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting, tulijaribu kuangalia mapungufu yetu na hatimaye tukafanyia kazi na kupata ushindi huu,” alisema.
Alisema wanajipanga kwa mchezo ujao kuhakikisha wanapambana na kupata matokeo mazuri.
Share:

Kiir akubali wanajeshi wa UN watumwe Juba, Sudan Kusini


Rais wa Sudan Kusini hatimaye amekubali kikosi cha ziada cha wanajeshi wa kulinda amani kitumwe nchini humo.
Rais Salva Kiir alichukua hatua hiyo baada ya kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Bw Kiir alikuwa awali amekataa kutumwa kwa wanajeshi hao 4,000 kutoka mataifa ya kanda, akisema huo ni ukiukaji wa uhuru wa Sudan Kusini.
UN iliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi hao baada ya kuzuka upya kwa vita baina ya wanajeshi waaminifu kwa Bw Kiir na aliyekuwa makamu wake wa rais Dkt Riek Machar mwezi Julai mjini Juba.
Kikosi hicho cha ziada kitakuwa na mamlaka zaidi kushinda kikosi cha sasa cha wanajeshi 13,000 ambacho kimekuwa kikihudumu nchini humo.
Share:

TAMWA YAPAMBANA NA AJALI KUOKOA MAISHA

AJALI za barabarani zinaua watu takribani milioni 1.25 duniani kila mwaka wakati hapa nchini takwimu zinaonesha katika ajali za miezi sita kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, watu 1,580 wameshapoteza maisha kutokana na ajali hizo.
Tawimu zilizotolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga zinaonesha kwamba marehemu hao 1,580 walitokana na ajali 5,152 ambapo watu waliojeruhiwa ni 4,659. Wanawake waliokufa kutokana na ajali hizo Kamanda Mpinga anasema ni 301.
Kati ya ajali hizo mkoa wa Mbeya ulikuwa unaongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi. Kutokana na kubainika kuwa ajali za barabarani zinachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake na watoto hapa nchini, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) kimezindua mradi unaolenga kupunguza ajali hizo.
Mradi huo ulizinduliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Kamanda Mpinga ambaye anabainisha kuwa idadi ya wanawake na watoto wanaokufa kutokana na ajali za barabarani ni kubwa, hivyo anawapongeza Tamwa kuanzisha mradi huo.
Lengo la mradi huo wa Tamwa ni kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wananchi ili kusaidia kuokoa wanawake na watoto na ajali hizo.
Katika uzinduzi huo inaelezwa kuwa ajali nyingi zinazotokea barabarani ni kwa sababu ya uzembe unaofanywa na madereva na watembea kwa miguu kwa kupuuza sheria za usalama barabarani.
Katika mradi huo Tamwa inajikita katika maeneo manne ambayo ni ulevi wakati wa uendeshaji vyombo vya moto, uvaaji wa kofia ngumu (helmet) kwa waendesha pikipiki na abiria, kufunga mikanda na mwendokasi. Mpinga anasema sheria nyingi za barabarani zinatakiwa zifanyiwe marekebisho kwani watu wameshazizoea na hawaziogopi tena.
“Sisi tunaona sheria zetu zina upungufu na watu wamezizoea. Dereva akipelekwa mahakamani adhabu yake ni faini au kifungo, lakini anakwenda mahakamani akiwa ameandaa kabisa faini kwani anajua atalipa na kuondoka. Tukiweka kifungo kama makosa mengine madereva watakuwa na nidhamu.
“Vifungu vya sheria kuwa legelege vinatoa mwanya kwa madereva kusababisha ajali kwa uzembe, hivyo uwepo wa sheria ambazo zinatoa adhabu kali kama vile kifungo itasaidia kupunguza ajali za barabarani," anasema.
Anasema ana imani kwamba mradi ulioanzishwa na Tamwa utasaidia kupunguza ajali kwa kiwango kikubwa katika miezi sita ijayo. Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga anasema wameanzisha mradi huo kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari katika kuufanikisha na hasa katika kusambaza elimu kwa umma. Sanga anasema baada ya kubaini wanawake na watoto wanaendelea kuangamia kwa ajali za barabarani zinazotokea kila siku nchini, Tamwa ikaona hilo si eneo la kupuuzia na hivyo kuanzisha mradi huo.
“Baadhi ya madereva huendesha magari yao bila kuzingatia sheria za barabarani na alama za mwendo gani wanatakiwa kuwa nao. Hata watembea kwa miguu wanapotumia barabara hawazingatii sheria. Mambo hayo yanachangia sana kusababisha ajali,” anasema.
Tatizo la unywaji wa pombe kwa madereva pia linatajwa kuwa ni sababu nyingine ya ajali za barabarani. Kiwango cha ulevi kinachoruhusiwa kwa madereva hapa nchini ni asilimia 0.08 ingawa ni kikubwa tofauti na kiwango kinachotambuliwa duniani cha asilimia 0.05.
“Waendesha bodaboda wamekuwa wakisababisha ajali wananchi wakiwemo wanawake na watoto kutokana na kukosa umakini, na ajali hizi husababisha vifo vingi kwa kuwa madereva na abiria wao hawavai kofia ngumu," analalamika Sanga.
Mtangazaji huyo mkongwe aliyewahi kuvuma TBC Taifa wakati huo ikiitwa Radio Tanzania, anasema ulevi kwa dereva, umuhimu wa kuvaa kofia ngumu kwa madereva na abiria wa bodaboda pamoja na kufunga mikanda katika mabasi na magari madogo ndivyo vitu ambavyo watajikita katika kuvitolea elimu.
Anasema watu wengi ambao ni abiria wa bodaboda wamekuwa wagumu kuvaa kofia ngumu kwa visingizio vya kuogopa kupata magonjwa ya ngozi bila kufikiria kuwa wanaweza kupata ajali mbaya, lakini kofia zikawaokoa kubaki walemavu au kufariki dunia.
“Kama watu wanaogopa kupata magonjwa kwa kuvaa kofia hizo basi wanatakiwa kuvaa kofia laini za plastiki na kisha kuvaa kofia ngumu kwa usalama wako,” anasema Sanga. Mratibu wa mradi huo kutoka Tamwa, Gladness Munuo, anasema mradi huo utakuwa endelevu ambapo wataanza kwa kukaa na madereva wa bodaboda na bajaji jatika jiji la Dar es Salaam na kisha kwenda mikoani.
“Mbali kutoa elimu kwa madereva, pia tutaongeza uelewa kwa waandishi wa habari katika suala la usalama barabarani kwa sababu wao wanasaidia katika kutoaji wa elimu,” anasema Gladness na kuongeza kuwa mradi huo pia utaangalia watembea kwa miguu.
Munuo anasema ajali za barabarani zinasababisha vifo vingi kuliko magonjwa na kwamba janga hilo ni la kimataifa ambapo takwimu zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua.
Anasema sababu zingine ambazo imegundulika kwamba zinazochangia ajali kuwa ni matumizi ya simu za kiganjani kwa dereva anapokuwa akiendesha gari, mwendo kasi, dereva kulazimisha kupita gari la mbele na kutokuwepo kwa alama za barabarani kwa baadhi ya maeneo.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Godfrey Sansa, anasema kutokana na hali ya kiuchumi, mwanamke ni mtumiaji mkubwa wa vyombo vya usafiri ambavyo sio salama na hususani pikipiki na bajaji.
“Wajasiriamali wengi tunaowaona mitaani ni wanawake, wanasafiri hapa na pale kwa usafiri wa pikipiki na bajaji kutokana na urahisi wa nauli. Kwa hiyo ni rahisi sana kwao kupata ajali. Wanawake pia tunawakuta barabarani wakiuza mihogo hivyo ni rahisi pia maisha yao kuwa hatarini,” anasema Dk Sansa.
Sansa anawaasa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kama chombo cha kuokoa maisha ya watu ambao wanateketea kwa ajali za barabarani katika kutafuta suluhisho la ajali na si kuishia kuripoti ajali na idadi za vifo. Pia anaishauri serikali kuwa na mfumo ambao utaweza kukusanya na kutoa taarifa sahihi za ajali kila zinapotokea.
“Hii itasaidia kufuatilia baada ya ajali ile, kwa mfano mtu huyo alikufa, familia yake ilibaki vipi? Kama hakufa aliumia pengine alipata ulemavu tujue anaishi vipi baada ya kupata ulemavu.”
Anasema katika suala hili kuwe na utaratibu wa kuihusisha pia jamii kuliko kutegemea taarifa za serikali pekee na taasisi zote zinazo tekeleza miradi ya aina moja kuwa na umoja katika kupambana na tatizo.
Share:

UWANJA WA KARUME PEMBA WAANZA KUTOA HUDUMA

UWANJA wa Ndege wa Karume uliopo Pemba sasa umeanza kutoa huduma za kutua na kuruka kwa ndege nyakati zote ikiwemo usiku.
Hali hiyo inatokana na matengenezo makubwa yaliyofanywa kwa kuweka taa za kuongoza ndege na zinazoruhusu ndege kutua nyakati za usiku, mradi unaotajwa kuigharimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zaidi ya Sh bil 1.6.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi (Gavu) alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zilizochukuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuona kisiwa cha Pemba kinapiga hatua ya maendeleo kiuchumi na katika sekta ya utalii.
Gavu aliyesimamia mradi huo wakati akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, alisema kukamilika kwa mradi huo ni fursa nyingine kubwa ya kukua kwa uchumi Pemba.
Aliyasema hayo wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli mwishoni mwa wiki kisiwani Pemba.
Baada ya kumaliza kuhutubia wananchi, Magufuli aliondoka kwa ndege kupitia katika uwanja huo akielekea Unguja pamoja na Dk Shein na viongozi wengine wa Zanzibar na wa Muungano.
Share:

MAMIA WAUAGA MWILI WA MKURUGENZI WA MAREHEMU A TO Z

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameongoza wakazi wa mkoa huo kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha A to Z , Anuj Shah, cha jijini hapa, kinachotengeneza vyandarua vyenye dawa.
Mwili wa Shah uliagwa jana na wafanyakazi wa kiwanda hicho, majirani wa kiwanda hicho, pamoja na rafiki zake kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Uliagwa katika makazi yake yaliyopo Kisongo na baadaye kuzikwa kwa kuchomwa moto kwenye makaburi ya Esso jijini hapa.
Akizungumza wakati wa maziko, Gambo alisema Shah alipenda kila Mtanzania mwenye nguvu apate ajira, ili kuendesha maisha ya familia yake, ndio maana aliamua kuajiri Watanzania walioishia darasa la saba na kuwafundisha kazi mbalimbali za ufundi kiwandani hapo.
"Niseme tu kuwa kampuni imepoteza mtu muhimu. Shah alikuwa na mapenzi makubwa na Watanzania na alitaka kila mtu apate ajira wakiwemo wanawake na wanaume, walemavu na wasio na ulemavu. Alikuwa rafiki wa familia yangu pia," Gambo alisema.
Aliutaka uongozi wa A to Z kuenzi maono ya Shah kwa kuongeza ajira zaidi ili kupunguza idadi ya Watanzania wasio na ajira.
Shah ni miongomi mwa waliogundua chandarua chenye dawa hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watu kutokana na ugonjwa wa malaria, husan mama wajawazito na watoto wanaotumia zaidi vyandarua hivyo.
Gambo aliongeza kuwa, katika kuonesha mapenzi yake kwa Watanzania, mwaka jana kwa kushirikiana na watafiti mbalimbali kupitia kituo chake cha utafiti cha ATRC, Shah aligundua mifuko ya kuhifadhia mahindi kwa muda mrefu bila kutobolewa na wadudu ikiwemo dumuzi.
Ilielezwa kuwa Shah alifariki dunia Septemba mosi mchana katika Hospitali ya MP Shah ya Jijini Nairobi alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na shinikizo la damu.
Share:

Thursday, 1 September 2016

JIONEE SIKU YA KUPATWA KWA JUA LEO SEPTEMBA 1, 2016

Wanafunzi wakiangalia kupatwa kwa jua kwa kutumia miwani maalumu.
TUMESHATANGAZIWA kuwa leo kutakuwa na kupatwa kwa jua. Kwa hapa Tanzania tukio hilo litatokea kati ya saa nne asubuhi na saa sita mchana.
Tukio hili ni la kawaida ambapo kivuli cha mwezi kinapokuwa kwenye eneo la dunia. Dunia inapolizunguka jua na mwezi kuzunguka dunia, hutokea mwezi ukakaa katikati ya jua na dunia katika mstari mnyoofu na kuzuia mwanga wa jua kufika duniani. Tukio hili hujulikana kama kupatwa kwa jua. Kwa kanuni za mwanga, kuzibwa kwa mwanga kutoka kwenye chanzo husababisha kivuli chenye sehemu mbili, Sehemu ya kwanza ni kivuli kikuu, yaani giza totoro (umbra) kikizungukwa na kivuli chenye mwanga mdogo au hafifu (penumbra).
Kwa sehemu ambayo kivuli cha mwezi ni hafifu huitwa kupatwa kwa mwezi kipete au kwa lugha ya Kiingereza ‘partial eclipse’ ili kukitofautisha na kile ambacho dunia inafunikwa kabisa (umbra) au kwa Kiingereza total eclipse of the sun. Kwa mwaka huu, kitakachoshuhudia nchini mwetu ni kupatwa kwa mwezi kipete (kuonekana kama pete) yaani kinachoitwa kwa Kiingereza, partial eclipse of the sun. Ni hali ambayo huwa haitokei mara kwa mara lakini kwa sasa dunia nzima hali hiyo itashuhudiwa maneo ya mikoa ya Njombe na Katavi.
Wako baadhi ya watu wanaohusisha kupatwa kwa jua na imani za kijamii. Kwa mfano, mjamzito anaambiwa akae ndani wakati wa tukio hilo ili mimba isiharibike. Wengine huhusisha kupatwa kwa jua na uchawi. Kwa wengi mliosoma mnajua kwamba hili ni tukio litokanalo na mizunguko ya magimba huko angani. Unaweza hata kutengeneza mfumo wa jua katika maabara na kuigiza (simulate) mzunguko wa dunia na mwezi na kuchunguza kivuli cha jua la kuigiza.
Vilevile mliosoma mambo haya bila shaka mnajua kwamba hili ni tukio ambalo halitokei mara kwa mara katika eneo moja. Inaweza kuchukua miongo au hata karne kabla halijarudia sehemu fulani. Kutokana na upotofu ambao uko kwenye baadhi ya jamii, kumekuwa na juhudi makusudi za kuelimisha umma kuhusu kupatwa kwa jua. Kwa mfano, Kituo cha televisheni cha Channel Ten wiki chache zilizopita kiliendesha kipindi kuhusu kupatwa kwa jua kutakakoonekana leo nchini mwetu.
Kituo hicho kiliwakaribisha wataalamu wa Fizikia ya Anga (Astrophysics) watatu akiwepo Dk Nooral Jiwaji kulizungumzia suala hilo. Dk Jiwaji ni mtaalamu ambaye hutuandikia sana makala za nyota katika gazeti la Daily News. Dk Jiwaji ameunda kikundi chake kiitwacho ‘AstroContact Group’ ambacho anatarajia kisaidie katika kuelimisha umma katika nyanja ya astronomia.
Katika mchango wake alipokuwa studio, Dk Jiwaji aliitaja siku ya kupatwa kwa jua kwa kusema, “Septemba 1 (yaani leo) kutakuwa na kupatwa kwa jua kipete kuanzia saa 2:13 hadi saa 8:00 mchana kutegemeana na na mahala utakapokuwa.” Alisema hivyo kwa kuwa dunia inajizungusha kwenye mhimili wake na kivuli kinahama sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu ya mzunguko huo.
Aliendelea kuwashauri watu wasitumie miwani ya jua, vionambali (telescopes), kamera n.k. kwa sababu mionzi ya jua ijulikanayo kama ‘ultraviolet rays’ inaweza kuharibu macho yao. Akasema badala yake watumie vioo maalumu vijulikanavyo kama ‘eclipse glasses’. Mmoja wa watazamaji alitaka kujua kama kupatwa kwa jua kuna athari kwa wanyama. Alijibiwa kwamba wakati mwingine kupatwa kwa jua huathiri wanyama wafugwao. Akasema kwa mfano, giza hilo huwafanya kuku warudi kwenye vibanda vyao wakihisi usiku umefika.
Lakini akasema, binadamu asiyekuwa na hii taaluma hujaa hofu hasa kama jua lilikuwa kali (bila mawingu) na ghafla giza likaingia. Wengine wanaotazama jua hilo dakika chache kabla ya kupatwa husema jua linapigana na mwezi. Mwanga wa jua unaporudi wanasema jua limeshinda! Juhudi nyingine ni zile za waandishi mbalimbali walioandika kuhusu kuwepo kwa tuko hilo la kupatwa kwa jua. Kwa mfano, mwandishi wa gazeti hili katika toleo la tarehe 22 Agosti 2016, Theopista Nsanzugwanko aliwakumbusha wasomaji kuhusu siku hiyo.
Pamoja na kutoa maelezo mafupi, alimnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hewa (TMA), Dk Agness Kijazi akisema: “Kiwango cha kupungua kwa joto wakati wa kupatwa kwa jua kunatofautiana kulingana na umbali kutoka katika eneo ambalo jua limepatwa.” Alisisitiza pia kwamba hakuna athari kubwa zinazotarajiwa kutokea. Mkoa wa Njombe ambapo zaidi ya asilimia 90 ya kupatwa kwa jua kutatokea, Dk Rehema Nchimbi, akizungumza na vyombo vya habari aliwaonya watu wasitazame jua wakati wa kupatwa bila kutumia vifaa maalumu.
Aliwaeleza wananchi watakaotaka kutazama jua kuwa vifaa hivyo vya kutazamia vinapatikana. Taarifa hii imetolewa mapema ili watu wajiandae kwa tukio hilo la kihistoria. Dk Nchimbi aliwakumbusha kwamba tukio hilo hutokea baada ya muda mrefu na linaweza lisirudie tena sehemu litakapotokea leo, yaani hapa Tanzania na badala yake likatokea sehemu nyingine ya dunia.


Kituo cha redio cha East African Radio, Agosti 29, kilitoa muda mwingi wa matangazo kuwaelimisha wananchi kuhusu tukio hilo. Lakini la msingi la kuzingatia ni watu kujua kwamba tukio hili si muujiza na kuepuka kuangalia jua bila kuvaa vifaa maalumu.
Share:

VITAMBULISHO VYA UTAIFA KUKOMESHA WAHAMIAJI HARAMU KIGOMA

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kabwe Zitto
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamelalamikia operesheni ya kukamata wahamiaji haramu inayoendelea mkoani Kigoma na kupendekeza kuwa ili kumaliza tatizo hilo, serikali haina budi kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mkoa huo.
Wakizungumza katika mkutano wa kujadili mpango wa Tushirikishane unaosimamiwa na Jamii Forum, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo, walisema kuwa ukamataji unaofanyika sasa, unakiuka haki za wananchi.
Diwani wa Kata ya Kigoma Mjini, Hussein Kalyango alisema, katika ukamataji huo ambao hufanywa na polisi wakati wa usiku, umekuwa ukinyanyasa raia kwani wakati mwingine wanaokamatwa huachiwa bila kupewa fidia yoyote baada ya kusota rumande kwa zaidi ya siku tatu na kufanyiwa unyanyasaji mwingine.
Diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini, Clayton Revocatus alisema, wameshalalamikia jambo hilo kwa uongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji mkoani Kigoma, lakini wamekuwa wakipata majibu ya vitisho na kukatisha tamaa, jambo linaloashiria kwamba unyanyasaji huo wa raia kwa tuhuma za uhamiaji haramu, hazitaisha katika siku za karibuni.
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Kabwe Zitto alisema, suala la uhamiaji haramu kwa wananchi wa mkoa huo, ni tatizo kubwa na walishaanza kulishughulikia kwa kufanya vikao na watu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), lakini mabadiliko ya viongozi wa taasisi hiyo yamefanya jambo hilo kutotekelezwa kwa sasa.
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mkoa wa Kigoma inamshikilia Ofisa Uhamiaji wa Wilaya Uvinza, Novat Kato (46) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Raphael Mbwambo alisema, mtuhumiwa huyo alipokea Sh milioni 8.1 Novemba mwaka jana, kutoka kwa wakulima kutoka Burundi, waliokuwa wakilima na kuishi nchini bila vibali kwa lengo kuwapatia vibali vya kuishi na kufanya kazi kinyume cha taratibu za utendaji wa idara hiyo.
Share:

VODACOM YATOA UFAFANUZI ONGEZEKO LA MAPATO

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imesema ongezeko la mapato ya Sh bilioni 1.9 halina uhusiano wowote na ufungwaji wa mtambo mpya wa kuratibu mapato ya kampuni ya simu au kodi ambazo hazijalipwa kipindi cha nyuma, bali limetokana na Sheria mpya ya Kodi ya Mwaka 2016.
Aidha, imefafanua kuwa katika kipindi kifupi mabadiliko hayo yataongeza pato la serikali, lakini mabadiliko hayo yanaonesha kwamba matokeo hayo yatapunguza watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kutokana na watumiaji kutomudu gharama.
Kampuni hiyo ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao, sheria hiyo mpya imeongeza wigo wa kodi katika sekta ya mawasiliano kwa kuongeza asilimia 10 ya kodi ya zuio katika kutoa fedha kwenye simu na sio makato ya kufanya miamala.
Alisema kutokana na watumiaji wake wengi kutoweza kumudu gharama zake na mapato yalioongezeka yatapungua, hali ambayo itarudisha nyuma jitihada za pamoja za kuwezesha Watanzania kuwa kwenye mfumo rasmi wa matumizi ya fedha.
“…ongezeko ambalo ni mbali na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo inakuwa tayari imelipwa. Matokeo ya ongezeko hili malipo yetu ya kodi yameongezeka kufikia shilingi bilioni 1.6 kwa mwezi,” alisema Ferrao.
Alisema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia pato la serikali na kushiriki kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia nyanja mbalimbali. Pia kampuni hiyo inaongoza katika sekta ya mawasiliano kwa kukusanya na kulipa kodi ya mapato nchini Tanzania.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Machi 2016, Vodacom Tanzania ilichangia zaidi ya Sh bilioni 367 katika makusanyo ya kodi za serikali.
Sekta ya mawasiliano nchini Tanzania ni ya pili kwa kutozwa kodi kubwa katika bara zima la Afrika hali ambayo inazidisha changamoto kwa wawekezaji wa sekta hiyo hususani katika kujenga miundombinu bora.
Sheria mpya ya fedha ya mwaka huu iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato kutoka katika kampuni za simu.
Share:

WATUMISHI 15 SIHA WAHOJIWA IKULU

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Valerian Jual, amesema watumishi 15 wa halmashauri hiyo wanaohojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokana na tuhuma mbalimbali.
Jual alitoa taarifa hizo juzi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadik, aliyetembelea wilaya ya Siha kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Alisema licha ya watuhumiwa hao, pia watumishi wengine watano walishikiliwa na jeshi la Polisi kwa kukosa dhamana wakituhumiwa kusafirisha jenereta tano zilizotumika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na vifaa vya pikipiki kwenda kusikojulikana.
Jual alisema, hadi sasa taasisi za serikali zinaendelea na uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao, kwa lengo la kumaliza uozo na ubadhirifu mali za serikali ambapo uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Tuhuma zinazowakabili watumishi hao (majina yamehifadhiwa), ni pamoja na kushindwa kuthibitisha uhalali wa malipo zaidi ya Sh milioni 70 ambazo ni fedha za uhamisho wa walimu, motisha, utengenezaji wa madawati na uchaguzi, fedha za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zaidi ya Sh milioni 50 na fedha za uchomaji takataka za uchaguzi huo Sh milioni 10.
Mkurugenzi huyo pia alikanusha uvumi unaoenezwa kuwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha, ndilo lililoibua tuhuma hizo, ambapo ameeleza haikuwa ajenda ya bazara hilo, bali ilikuwa ni ajenda ya taasisi za serikali ya siku nyingi katika kusafisha halmashauri zote nchini ikiwamo ya Siha.
"Tangu nilipokabidhiwa ofisi, ndipo taasisi za serikali ziliingia ofisini kwangu kwa ajili ya kufanya uchunguzi na sio ajenda ya baraza la madiwani kama inavyodaiwa, katika uchunguzi huo nimepata ushirikiano mzuri sana katika taasisi za serikali hususani ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo," alisema Jual.
Share:

NINA IMANI NA VIONGOZI WALIOCHAGULIWA KWA HAKI

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) anayemaliza muda wake, ambaye pia ni Rais wa Botswana, Dk Seretse Kahama Ian Khama, amempongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana.
Rais huyo wa Botswana alitoa pongezi hizo kupitia hotuba aliyoitoa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC unaofanyika Mbabane- Swaziland ambako Dk Magufuli anawakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Dk Khama alisema, ukuaji wa demokrasia katika nchi wanachama wa SADC unaendelea kuimarika hivyo ni muhimu jitihada hizo zikaendelezwa zaidi.
Amesema, ana imani na viongozi waliochaguliwa kwa njia ya amani, uhuru na haki katika ukanda wa SADC akiwemo Rais wa Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli kwamba watafanya kazi kwa bidii kuharakisha maendeleo kwa wananchi wao.
Viongozi wa nchi za SADC waliokuwa katika mkutano huo walishuhudia zawadi mbalimbali zikitolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye utunzi wa insha na kwa wanahabari walioandika habari mbalimbali kuhusu SADC, ikiwemo masuala ya huduma ya maji.
Aidha, katika mkutano huo wa 36 wa SADC, viongozi wanaohudhuria watafanya uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama ( SADC Troika).
Katika mkutano huo, wakuu wa nchi na Serikali watapokea rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali kutoka kwenye Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutia saini.
Miongoni mwa rasimu hizo ni mkataba wa kuboresha Itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya Itifaki ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC na maboresho ya Itifaki ya Biashara.
Share:

KIDATO CHA 5 AWAMU YA PILI 2016

TAARIFA KWA UMMA

31-AUG-2016.


OR-TAMISEMI inatangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya Pili (Second Selection) kwa mwaka 2016. Jumla ya wanafunzi 3,918 wakiwemo wasichana 2,413 na wavulana 1,505 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza.
Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 1,864 wakiwemo wasichana 1,099 na wavulana 765 sawa na asilimia 47.58 watajiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati; na wanafunzi 2,054 wakiwemo wasichana 1,314 na wavulana 740 sawa na asilimia 52.42 wamechaguliwa kusoma masomo ya Sanaa na Biashara.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2015 wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili atakuwa amepoteza nafasi hii.
Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016 inapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz
Imetolewa na Katibu Mkuu,
OR-TAMISEMI

bofya hapa: http://tamisemi.go.tz/noticeboard/tangazo-1060-20160901-Waliochaguliwa-kujiunga-kidato-cha-tano-awamu-ya-pili-2016/second-selection-2016.pdf
Share:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba