Thursday, 27 October 2016

Ofisa usalama feki atupwa jela miaka 2

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.
Hata hivyo, mahakama imetoa hukumu hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa mashitaka, ulileta mashahidi wanne kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma hizo.
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo na kwamba mahakama inamtia hatiani mshitakiwa licha ya yeye kutokuwepo.
“Hati ya kumkamata mshitakiwa itolewe na adhabu hii itaanza kutumika pindi mshitakiwa atakapokamatwa kwani alitoroka akiwa na haki ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.
Inadaiwa kuwa Novemba 19, 2014 maeneo ya Kariakoo Msimbazi wilayani Ilala, mshitakiwa alijitambulisha kwa Issaya Odelo na Charles Odinga kuwa Ofisa Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua si kweli. Katika hatua nyingine, kondakta Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba daladala.
Mbali na mshitakiwa huyo, Exavery Kaunga (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa baada ya ushahidi dhidi yake kuwa na shaka.
Akitoa hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, alisema kuwa upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne kuthibitisha kosa hilo.
“Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, nakutia hatiani mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela,” alisema Hakimu Hassan.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa ni kwa nini asipewe adhabu kali, hakujibu chochote na mahakama kutoa adhabu hiyo.
Washitakiwa hao walishitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka jana, washitakiwa walikula njama kutenda kosa.
Pia inadaiwa Julai 5,2015 pembezoni mwa barabara ya Nyerere katika Kituo cha Mafuta cha Victoria, washitakiwa waliiba gari lenye namba za usajili T 624 CSH aina ya Eicher mali ya Kampuni ya White Swan.
Share:

TFS yanasa lori lenye shehena ya mbao

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wamekamata lori lililokuwa likisafirisha mbao zilizovunwa kinyume cha sheria baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria.
Lori hilo lenye namba za usajili T 676ANQ aina ya Scania lililokuwa likitoka Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam, lilikutwa limetelekezwa katika maegesho ya mkazi wa Dar es Salaam, eneo la Amana katika Manispaa ya Ilala na dereva wa lori hilo kutokomea kusikojulikana.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kuzibaini mbao hizo kutokana na kufunikwa kwa miche ya sabuni, viroba vya dawa za kuku pamoja na chupa tupu zilizokuwa zimeshatumika.
Kaimu Ofisa Habari ambaye pia ni Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala hao, Nurdin Chamuya alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria kuwa kuna lori limebeba mbao zilizovunwa kiharamu, walishirikiana na kikosi maalumu dhidi ya ujangili wa wanyama pori na kubaini lori hilo likiwa limetelekezwa katika eneo hilo.
Alisema wanamtafuta dereva wa lori hilo pamoja na mmiliki wake ili sheria ichukue mkondo wake huku akitoa mwito kwa wananchi kufuata taratibu na sheria za uvunaji wa miti ya mbao ikiwa ni pamoja na kuwa na vibali halali vinginevyo atakayebainika atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi.
Share:

Kiini cha nauli juu Dar-Zanzibar chaelezwa

TATIZO la uhaba wa vyombo vya usafiri kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ikiwemo boti zinazokwenda kwa kasi, kwa kiasi kikubwa kumechangia kuwepo kwa tatizo la ulanguzi wa tiketi kwa abiria na kusababisha usumbufu mkubwa.
Ulanguzi wa tiketi hizo umeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi, Mohammed Ahmada wakati alipofanya ziara katika eneo la bandari ya Malindi.
Tiketi moja ya boti zinazokwenda kwa kasi zinazomilikiwa na Kampuni ya Azam Marine inayouzwa Sh 20,000 hupanda bei na kufikia Sh 30,000 hadi 40,000.
Ahmada, akizungumza jana alionesha kukerwa na tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi kwa sababu linaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi, wakiwemo kinamama na wazee.
Alisema ingawa tatizo hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vyombo vingi vinavyofanya safari kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, lakini isiwe sababu ya kupandisha bei kwa kiwango hicho na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Meneja wa Usafiri wa Kampuni ya Azam Marine, Ali Mohamed Abeid alikiri kuwepo kwa tatizo la tiketi za magendo ambalo wamekuwa wakipambana nalo kwa kiwango kikubwa.
Share:

Serikali yazindua mpango maalumu kuboresha afya

SERIKALI imezindua mpango maalumu kitaifa wa kuboresha afya ujulikanao kama Mkoba wa siku 1,000 utakaotumika kutekeleza afua mbalimbali za lishe nchini kwa lengo la kupunguza udumavu kwa watoto na upungufu wa damu kwa wajawazito na wanyonyeshao.
Mkoba wa siku 1,000 ni nyenzo ya uwezeshaji unaotumia njia mbalimbali za mawasiliano yenye lengo la kushawishi mabadiliko ya tabia na mitazamo kuhusu lishe katika jamii, ukihamasisha wajibu wa kijinsia wa wazazi na walezi walio ndani ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mwanadamu ambazo zinahesabiwa tangu mimba inapokuwa imetungwa hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili.
Akizindua mpango huo jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Zainab Chaula alisema Mkoba wa siku 1,000 utaasiliwa na serikali kama Mkoba Maalumu wa Kitaifa.
Alisema mpango uliotengenezwa na mradi wa lishe wa Mwanzo Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) ulifanya kazi katika mikoa sita nchini ambao umesaidia pia kupunguza tatizo la udumavu.
Kuhusu udumavu, Dk Chaula alisema ni jambo lililopo lisiloonekana ingawaje ni hatari likiwa tishio kijamii, kiuchumi na likihitaji kufanyiwa kazi na kupatikana kwa suluhu.
Alisema serikali imejipanga kuratibu juhudi zilizofanywa na wadau katika kupambana na aina yoyote ya udumavu nchini.
Alisema Mkoba wa siku 1,000 utatumiwa na wadau mbalimbali kama maofisa lishe wa wilaya na mikoa, wahudumu wa afya katika jamii ili kuchochea tabia chanya zinazolenga kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa wajawazito na wanaonyonyesha na udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili.
Alisema msisitizo umewekwa katika kuboresha matendo na majukumu katika jamii ambayo ni muhimu sana katika kupunguza matatizo ya lishe kwa akina mama na watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dk Joyceline Kaganda alisema Mkoba wa siku 1,000 una vyumba sita kila kimoja kikiwa na alama maalumu ya utambulisho, kila chumba kimehifadhiwa machapisho mbalimbali yenye jumbe zinazohamasisha matendo na tabia chanya za lishe katika kila hatua ya maendeleo ya ukuaji wa mtoto.
Share:

Wanaosomea fani za kipaumbele wapewe mikataba

TAARIFA kwamba serikali inakusudia kuweka utaratibu wa kuwabana wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za kipaumbele, kutumikia utumishi wa umma kwa muda fulani, haina budi kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo ya kweli.
Fani ambazo serikali kwa makusudi imezipa kipaumbele kwa lengo la kupata wataalamu wa kutosha katika maeneo husika, ambayo kwa sasa yana wataalamu wachache ni pamoja na fani za sayansi ya tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta, gesi asilia, sayansi asilia, mabadiliko ya tabia nchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alidokeza juu ya kusudio hilo la serikali, alipokuwa anazungumzia hivi karibuni juu ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Alisema serikali inafikiria kuchukua hatua hizo, kutokana na kubaini kuwepo kwa wanafunzi wanaosomea fani hizo kwa lengo la kupata mikopo, lakini wakishahitimu hukimbilia kufanya kazi nyingine; au kwenda kufanya kazi nje ya nchi, hivyo kuzorotesha lengo la kupata wataalamu waliotarajiwa katika fani husika.
Ni wazi kwamba kwa mtindo huo, lengo la serikali la kutoa kipaumbele kwa fani hizo, litaendelea kukwamishwa na wanafunzi wenye azma ya kupata mikopo zaidi kuliko kukuza fani husika kwa kuongeza idadi ya wataalamu wake.
Sisi tunaunga mkono pendekezo la serikali kwamba wanafunzi wanaotaka kuingia katika fani hizo na kupewa kipaumbele katika mikopo, waingie mkataba na serikali kwa muda maalumu wa kutumikia umma ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuwapa kipaumbele inatimia.
Tungependa kukumbushana tu kwamba jambo hilo siyo geni hapa nchini kwetu, kwani miaka ya nyuma taasisi na mashirika ya umma, yaliweza kuwasomesha wafanyakazi wao kwa kuwalipia gharama zote za masomo na malazi katika vyuo mbalimbali ndani na hata nje ya nchi.
Lakini hiyo ilikuwa inafanyika kwa utaratibu maalumu, ambapo mfanyakazi alikuwa akiingia makubaliano ya kisheria kwamba atakapohitimu, atalazimika kulitumikia shirika husika, siyo chini ya miaka miwili au mitatu, kabla ya kuamua kuondoka na kwenda kufanya kazi nje ya shirika husika.
Wengi walisomeshwa kwa utaratibu huo; na walioondoka baada ya kuhitimu, walichukuliwa hatua kali kwa mujibu wa makubaliano waliyoyafikia hapo awali na waajiri.
Wakati umefika sasa kwa vijana wetu, ambao serikali imeamua kuwapa kipaumbele katika kupata mikopo kusomea fani hizo ili kupunguza pengo la wataalamu, nao wakaingia katika mkataba maalumu na serikali kuutumikia umma baada ya kuhitimu masomo yao kwa muda fulani.
Mkataba huo maalumu utawafanya vijana hao, wawajibike kama tunavyotarajia, badala ya kutumia mkopo na kisha kujiondokea pasipo utaratibu. Hali hii ni sawa na matumizi mabaya ya rasilimali ya umma, jambo ambalo asilani lisifumbiwe macho.
Share:

Polisi yawashikilia wanne mtandao wizi wa magari

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za wizi wa magari kwa kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema jana Dar es Salaam kuwa askari waliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Watuhumiwa hawa wanajihusisha na wizi wa magari kwa mbinu ya kununua nyaraka za magari yaliyopata ajali na kulipwa na bima, pamoja na kukata vibali vya namba ya ‘chassis’ ya magari hayo kisha kuweka kwenye magari waliyoyaiba,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema baada ya askari kupata taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji eneo la Tandale na kukamata mtuhumiwa Dennis Gasper (25), mfanyabiashara wa Manzese Uzuri akiwa na mabaki ya gari namba T 290 DDM Toyota ALPHAD.
Alisema katika mahojiano mtuhumiwa alitaja watuhumiwa wengine na kuwaongoza askari hadi Magomeni Mikumi maeneo ya kituo cha daladala na kuwakamata watuhumiwa wengine watatu ambao ni Alfred Ditrick (33), mkazi wa Sinza, Venance Bureta (24) wa Mbezi na Dickson Valentino (23) mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na mkazi wa Kimara, wote katika Jiji la Dar es Salaam.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikutwa na gari la wizi namba T 368 CES Toyota Passo na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya wizi wa magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuyauza nje ya mkoa huo.
Katika tukio lingine, askari wamekamata magari mengine matatu ya wizi yaliyoibwa mkoani Dar es Salaam na kupelekwa mafichoni Arusha yakiwemo Toyota Vitz T 262 CTF, Suzuki Carry lenye namba za usajili T 935 CPC, Toyota Passo lenye namba za usajili T 368 CES na Toyota Landcruiser Prado lenye namba za usajili T 735 BLZ.
Alisema watuhumiwa wa mtandao huo wanashikiliwa mkoani Arusha na juhudi za kuwafuata zinafanyika ili kuja kuwaleta Dar es Salaam kujibu mashitaka yanayowakabili.
Share:

Pluijm aziita timu zinazomtaka

KOCHA Hans van Pluijm amesema milango iko wazi kwa timu yoyote inayomhitaji.
Kocha huyo Mholanzi alitangaza kujiuzulu juzi baada ya waajiri wake Yanga kuingia mkataba na kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina bila kumshirikisha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alikiri timu kadhaa kumwania lakini akasema ni mapema kuzitaja na kusisitiza amefungua milango kwa yeyote inayomtaka kumfuata kwa mazungumzo.
“Muhimu siwezi kukaa bila kufundisha kwa sababu ndio kazi yangu na nimeizoea hivyo kweli nahitaji timu ya kufanya nayo kazi,” alisema.
Licha ya kujiuzulu, taarifa za Yanga zilisema kuwa Pluijm alitakiwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na nafasi yake ya ukocha angepewa Lwandamina, jambo ambalo Pluijm alilikataa.
“Nahitaji kuendelea kufundisha timu yoyote itakayonihitaji, ni mapema kuzungumzia ni wapi, lakini nawashukuru Yanga na wachezaji wote kwa kipindi chote ambacho tulifanya kazi pamoja, pia mashabiki waendelee kuiunga mkono timu yao wasikate tamaa,” alisema.
Pluijm amekuwa akihusishwa na kujiunga na Azam FC, jambo ambalo amelikanusha kuwa halina ukweli.
Alisema sio vyema kuzungumzia timu ambayo tayari ina makocha wake, kitaalamu haipendezi. Kwa upande wa Azam FC walisema kwa sasa hawana mpango wa kumbadilisha kocha, kwani aliyepo bado ana mkataba, na kwamba wanaamini wachezaji watamuelewa taratibu falsafa yake na mambo yatakwenda vizuri.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema jana kuwa Pluijm ni kocha mzuri na anasikitika kuondolewa kwake katikati ya ligi na kwamba anamheshimu isipokuwa hawana mpango wa kumchukua.
“Tunaamini kocha tuliye naye ( Mhispania Zeben Hernandez) anatosha, naamini wachezaji wakimuelewa watabadilika na kufanya vizuri, kama itatokea kumbadilisha kocha basi tutaangalia sehemu nyingine na sio nyumbani,”alisema.
Share:

Serikali yazipiga stop Yanga, Simba

SERIKALI imezipiga stop klabu za Yanga na Simba kuendelea na michakato yao ya kubadili umiliki wake hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya katiba zao.
Hayo yalitangazwa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni klabu hizo kongwe ziliazimia kuingia kwenye mabadiliko, Yanga ikikodishwa na mwenyekiti wake Yusuf Manji na Simba ikitaka kuuza hisa asilimia 51 kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
Kiganja alisema Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji katika klabu hizo pamoja na nyingine za wanachama, ila inachotaka kwanza kufanyike marekebisho ya katiba zao kwani za sasa haziruhusu mabadiliko hayo.
Alisema kuwa BMT inapenda kuona wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Hivi karibuni kumeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…,” alisema.
Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua nyingi za wanachama wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 Ibara ya 56 inaeleza kuhusu kampuni ya umma: Inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young African Sports Corporation Limited ambayo itasajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama kampuni ya umma yenye hisa.
Sehemu ya pili ya ibara hiyo inasema wanachama wote katika klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2007 wako hai kwa nguvu ya uanachama wao watakuwa wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakapopata kwa mujibu wa muafaka wa Yanga uliofikiwa na wana Yanga Juni 22, 2006.
Klabu itamiliki hisa zilizosawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika klabu hiyo. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili, ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.
Tayari Yanga iko chini ya Kampuni ya Yanga Yetu ambayo ni mali ya mwenyekiti wa klabu hiyo Manji, ikiwa ni kinyume na katiba yao wenyewe.
Kiganja alisisitiza kuwa klabu zisitishe mipango ya kubadilisha uendeshaji na ziendelee kuwa mali ya wanachama. Wakati Yanga walikuwa tayari wameishaingia mkataba wa miaka 10 wa
kuikodisha klabu yao, wenzao wa Simba walijipa miezi sita kukamilisha taratibu za kuuza hiza.
Share:

Mbarawa awataka Posta kukusanya mapato

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania kusimamia mapato kwa kukusanya fedha kinyume cha hapo atachomoa mmoja mmoja na kuweka wengine kwa nusu saa tu.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo, alisema kwa kuwa serikali inahitaji fedha, kama waziri hahitaji kuambiwa maneno mengi, kwani tofauti na hapo ataendelea kuwachomoa wajumbe hao mpaka apate kile anachokihitaji.
“Nahitaji pesa kwenye shirika. Ukiniambia maneno mengi mimi sijali, mimi nataka pesa, serikali inataka pesa, sitaki kitu kingine. Ni lazima msimamie mapato mkishindwa nachomoa mmoja mmoja. Naweza kufanya hivyo nusu saa tu. Nitaendelea kufanya hivyo mpaka nihakikishe Napata kile ninachokihitaji,” alisema Profesa Mbarawa.
Share:

Historia MOI upasuaji kwa wenye kibiongo

KIBIONGO ni tatizo la kupinda kwa mgongo upande moja hasa wa kulia, hali inayomfanya mtu aliye na hali hiyo kutembea akiwa ama ameinama au kujikunja. Tatizo hilo mtu huweza kuzaliwa nalo au kutokea baadaye mtoto anapokuwa amefikisha umri wa miaka mitatu na kuendelea.
Kwa kuwa hapa nchini kulikuwa hakuna upasuaji kwa tatizo hilo, watu waliokuwa na shida hiyo walikuwa wakikua nalo hivyo hivyo isipokuwa wenye uwezo wa kifedha na kuwa na taarifa sahihi walipelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. Hivi sasa ufumbuzi umepatikana nchini.
Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji mkubwa kwa mafanikio wa kunyoosha mfupa wa mgogo wa mtoto uliopinda (kibiongo). Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma anasema upasuaji huo umefanyika kwa kutumia teknolojia ijulikanayo kama ‘posterior instrumentation and fusion’.
Inahusisha uwekaji wa vyuma maalumu kwenye mfupa wa mgongo katika sehemu ya juu na chini ya mfupa wa mgongo na kuufanya unyooke kama inavyotakiwa.
Dk Othman anasema taasisi hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji huo kupitia madaktari bingwa walioko kwenye mafunzo ya ubobezi wa juu katika upasuaji wa mifupa na mgongo kwa watoto kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Marekani.
“Uanzishwaji wa upasuaji huu umetokana na kuanzisha ushirikiano wa kimafunzo kati ya Taasisi ya MOI na Chuo cha Madaktari bingwa wa upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA) na madaktari bingwa kutoka Marekani,” anasema.
Anasisitiza kuwa uanzishwaji huu wa kunyoosha migongo ya watoto iliyopinda unatarajiwa kuisaidia serikali kupunguza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi ambazo ni za gharama kubwa.
Kutokana na hatua hiyo, uongozi wa MOI unatoa mwito kwa madaktari wote nchini kwenda kupata mafunzo hayo kwenye taasisi hiyo. Pia wazazi wenye watoto wenye matatizo hayo wawapeleke hospitalini wafanyiwe uchunguzi na upasuaji.
Awali watoto waliokuwa wakienda India na sehemu nyingine kutibiwa iliwagharimu dola 6,000 (Sh milioni 13 na zaidi).
“Sasa hivi upasuaji huo unafanyika hapa nchini, mgongo unanyooka na mgonjwa anarudi katika hali ya kawaida kwa gharama ya dola 2,000 tu (takribani Sh 4,400,000),” anasema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Viungo, Bryson Mcharo anasema huo ni upasuaji mpya, na ni mara ya kwanza kufanyika MOI lakini umekuwa ukifanyika nchi nyingine.
Anasema ukubwa wa kupinda kwa mgongo huo hutegemeana na umri wa mtoto. Anasema wataalamu hawajabaini sababu ya tatizo hilo. Mcharo anasema hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika upasuaji huo, na hivi sasa yupo kwenye mafunzo ya upasuaji wa mifupa ya watoto.
Katika upasuaji uliofanyika nchini, anasema walifanikiwa kunyoosha mgongo wa mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma kidato cha kwanza. Anasema kwa sasa Moi wana vifaa vinavyowawezesha kuwawekea wagonjwa 30 baada ya kufanyiwa upasuaji.
Inaelezwa kwamba baada ya mtu kufanyiwa upasuaji huo na kuwekewa kifaa maalumu mgongoni, kuna baadhi ya vitu hataweza kuvifanya tena kama awali.
Hupewa masharti ya kutoinama endapo anataka kuokota kitu ama kupinda kama wengine wanavyoweza na pia huelekezwa namna ya kuishi na kifaa hicho mwilini. Mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Yombo, Temeke, Dar es Salaam, Itika Mwankenja anasema mtoto wake hakuzaliwa na tatizo hilo na kwamba lilimpata akiwa na umri wa miaka 11.
“Kama wazazi tuligundua hali hiyo ya mabadiliko kwa mtoto wetu kwa kuwa ni kitu ambacho hatukuwahi kukiona kwake,” anasema.
Mzazi huyo anamshukuru Mungu kwa kumwezesha mtoto wake kufanyiwa upasuaji mkubwa wa mafanikio. Kwa mujibu wa mama huyo hivi sasa kuna tofauti kubwa kabla ya upasuaji na baada ya mtoto kufanyiwa upasuaji huo.
Anasema mtoto wake huyo anaendelea vizuri na mazoezi anayoyafanya baada ya upasuaji huo. Mtoto huyo anayesoma kidato cha kwanza anasema baada ya kupatwa hali hiyo, alikuwa akichoka anapokaa kwa muda mrefu hasa akiwa darasani.
“Ilibidi niwe najikaza ili muda wa kurudi nyumbani ufike na nilikuwa ninaandika kwa shida lakini kwa sasa baada ya upasuaji naweza kukaa muda mrefu,” anasema.
Ni dhahiri kwamba, MOI imeandika historia mwaka huu ya kufanya upasuaji mkubwa wenye mafanikio, hatua inayotajwa kuwa ni ukombozi kwa jamii ya Tanzania na majirani zetu.
Share:

Mfumo wa PReM utakavyodhibiti wanafunzi hewa

TANGU serikali iliporuhusu mazingira ya soko huria katika sekta ya elimu, kumekuwapo na shule binafsi nyingi. Katika shule hizo binafsi, suala la kuhamisha wanafunzi limekuwa halizingatiwi kama ilivyokuwa miaka ya nyumba ambapo ilikuwa ni lazima taarifa za mwanafunzi za kuhama zipate baraka na mamlaka za elimu katika ngazi za kata, wilaya na mkoa na taarifa kubaki katika ngazi hizo.
Kukatika kwa mnyororo huo ulifanywa uhamishaji na taarifa za mwanafunzi kutokuwepo katika ngazi husika zaidi ya shule ambayo mwanafunzi husika anatoka na kuhamia. Badala yake shule ambayo imepokea mwanafunzi ilikuwa ikiandika barua Necta ya kuainisha wanafunzi waliohamia na shule walizotoka.
Ili kuwa na mfumo unaoeleweka, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limeunda mfumo wa kutunza taarifa za wanafunzi wa Shule za Msingi (PReM) ambao utasaidia katika uandikishaji wa wanafunzi wote wa shule za msingi na wanafunzi hao kupewa namba maalumu itakayomtambulisha mwanafunzi katika ngazi mbalimbali za mafunzo zinazosimamiwa na baraza.
Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi anasema mbali na mfumo huo kumtambulisha mwanafunzi, pia utasaidia katika uhamisho wa mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine ndani na nje ya mkoa katika shule za umma na zile binafsi.
“Ni mfumo ambao utarahisisha utaratibu unaotumika sasa wa kuhamisha mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine ili kuondoa tatizo la wanafunzi hewa,” anasema. Anasema Mfumo wa PReM utasaidia katika uandaaji na utoaji wa takwimu za wanafunzi katika ngazi ya shule, wilaya, mkoa hadi ngazi ya kitaifa.
Aidha, Nchimbi anasema mfumo huo pia utasaidia katika ufuatiliaji wa taarifa za matokeo ya kila mwanafunzi kuhakikisha wadau mbalimbali wa elimu wanapata ufahamu wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya shule.
Baraza limefanya majaribio ya mfumo huu katika mikoa miwili ya Mwanza na Ruvuma na ifikapo Desemba mwaka huu, utaimarishwa ili Januari hadi Mei 2017, utumiwe na mikoa yote kusajili wanafunzi wa shule za msingi.
“Mfumo huu wa PReM utasimikwa Baraza la Mitihani Tanzania na kutumiwa na wadau mbalimbali wa Elimu. Baraza la Mitihani la Tanzania litahakikisha mfumo huu unapatikana katika ngazi za wilaya ili wadau wote waweze kupata taarifa mbalimbali za elimu,” anasema.
Anasema NECTA ina wajibu wa kutoa mafunzo ya uendeshaji wa mfumo wa ngazi ya mkoa, kuandaa na kusimamia taratibu za uandikishaji na utunzaji wa taarifa za mwanafunzi katika ngazi ya wilaya na mkoa, na kuchukua taarifa za usajili za wanafunzi wa darasa la nne na la saba.
“Necta pia ina wajibu wa kuweka matokeo ya mitihani ya kitaifa, kutatua changamoto za mfumo wa PReM katika ngazi ya mkoa, kuhakikisha usalama wa taarifa zilizohifadhiwa katika mfumo na kusimamia uendeshaji wa mfumo katika ngazi zote.
Aidha, Nchimbi anasema ili kufikia malengo mahususi ya mfumo wa PReM, kila mdau wa elimu atatakiwa kutimiza wajibu wake. Wadau hao ni mwalimu mkuu, mratibu wa elimu kata, ofisa elimu wilaya, mkoa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Anasema kwa ofisi ya mwalimu mkuu, inawajibu wa kuandaa orodha ya wanafunzi kwa ajili ya kuandikishwa kwenye mfumo wa kupeleka wilayani, kupeleka taarifa za uhamisho na matokeo ya kila mwaka kwa wanafunzi wote wilayani na kupokea ripoti za uandikishwaji na uhamisho wilayani.
Nchimbi anasema kwa upande wa ofisi ya mratibu wa elimu kata, ina wajibu wa kutoa ripoti za takwimu za shule katika kata husika, na kusimamia uingizaji wa taaria za wanafunzi ngazi ya shule na kata.
“Ofisi ya Ofisa Elimu wilaya yenyewe ina wajibu wa kusimamia uingizaji wa taarifa ya uandikishwaji, uhamisho na matokeo kwenye mfumo, kuthibitisha uhamisho wa mwanafunzi kwenye mfumo na kutoa ripoti za takwimu za shule zote wilayani.
Nchimbi anasema ofisi ya elimu mkoa, wanawajibu wa kutekeleza mfumo wa PReM kwa kusimamia uandikishwaji wa wanafunzi wa shule zote katika mkoa husika, kuthibitisha uhamisho wa mwanafunzi katika shule zote za mkoa husika na kutoa ripoti za takwimu za shule za mkoa husika.
Anasema kwa upande wa Ofisi ya Rais, Tamisemi inawajibika kuhakikisha kila mkoa unaingiza taarifa za wanafunzi wa ngazi zote katika shule za msingi na kutoa ripoti mbalimbali za takwimu na matokeo kulingana na mahitaji yao.
Nchimbi anasema wanawajibika pia kupokea na kuingiza taarifa za uandikishaji kutoka shule za wilaya na kuingiza taarifa za matokeo na uhamisho kwenye mfumo na kutoa ripoti za uandikishaji na uhamisho za kila shule katika wilaya husika.
Share:

Yanga siku 5 bao kumi

ANGA siku tano bao 10! ndivyo ilivyotokea jana baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu kushinda mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu na hivyo kuwa na mabao 10 ndani ya siku tano baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 6-2 Jumamosi iliyopita.
Ushindi huo uliopatikana kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam umeifanya Yanga kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 24, tofauti ya pointi tano na vinara wa ligi hiyo, Simba. Katika mechi hiyo ya kiporo, Yanga ilitawala katika vipindi vyote vya mchezo.
Obrey Chirwa nyota yake iliendelea kung’ara jana baada ya kufunga bao la kuongoza katika dakika ya tano ya mchezo huo.
Alifunga bao hilo kwa shuti baada ya kuunganisha mpira wa Simon Msuva. Mshambuliaji huyo sasa amefikisha mabao matano. Amisi Tambwe aliifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 63.
Alifunga bao hilo baada ya kuukokota mpira nje ya 18 huku mabeki ya Ruvu wakimsindikiza kabla ya kuachia fataki lililojaa wavuni. Dakika ya 82, Msuva alifunga bao la tatu kwa kazi nzuri ya Tambwe aliyempigia pande murua.
Tambwe aliibua tena shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kufunga bao la nne katika dakika ya 90 baada ya kumzidi ujanja mlinzi wa Ruvu, Michael Aidan aliyekuwa akirudisha mpira kwa kipa wake na Tambwe kuuwahi na kuujaza wavuni.
Share:

Kagera yatumia mil. 800/- ukarabati miundombinu

UKARABATI wa miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera umeanza, na tayari Sh milioni 800 zimetumika kati ya Sh bilioni tano zilizotolewa na wadau mbalimbali katika kuwachangia waathirika wa tetemeko hilo lililotokea Sept 10, mwaka huu na kusababisha vifo, uharibifu wa majengo na miundombinu mbalimbali.
Aidha, imeelezwa kuwa, inahitaji miaka miwili au mitatu kwa mkoa huo kurejea katika hali ya kawaida kutokana na maeneo mengi kuathirika vibaya.
Hayo yalibainishwa mjini Dodoma jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohammed Mchengerwa alipokuwa anazungumzia taarifa ya serikali ya maafa ya tetemeko yaliyotokea mkoani Kagera.
Taarifa hiyo iliwasilishwa mbele ya kamati hiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. Alisisitiza kuwa, serikali imeihakikishia kamati hiyo kuwa inaendelea na jitihada za kusaidia waathirika hao.
Aidha, alisema kwa mujibu wa taarifa ya waziri huyo kwa sasa wanafunzi wa shule ya sekondari Ihungo wamehamishwa kupelekwa shule ya Mwani ili kuendelea na masomo.
“Hadi sasa wagonjwa 440 waliokuwa hospitali wameendelea kupatiwa matibabu na kati ya wagonjwa hao sita wamefariki dunia,” alisema Mchengerwa.
Alisema kutokana na taarifa hiyo, kwa sasa idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko hilo imeongezeka kutoka watu 17 na kufikia 23.
Alisema taarifa hiyo pia imebainisha kuwa wananchi walioathirika na janga hilo, kwa sasa wanaendelea kupata huduma mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu yao ambapo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) takribani 96 wapo mkoani humo wakiendelea kulinda na kusaidia masuala ya usalama.
Akizungumzia mapendekezo ya kamati hiyo kwa serikali, Mchengerwa alisema imeitaka serikali kusimamia masuala ya afya na usalama kwa wananchi waliopatwa na tetemeko.
Aidha, alisema kamati hiyo imeishauri serikali iendelee kuratibu kwa kushirikiana na wahisani na kuhakikisha wanawatumia wataalamu wa ndani katika kufanya utafiti katika maeneo yenye bonde la ufa kabla ya maafa kutokea.
Pia kamati imeiomba serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya tetemeko na kujenga nyumba imara zinazostahimili mtikisiko, kuboresha kitengo cha maafa na kuanzisha vituo vya kitaifa vyenye vifaa vya kisasa vya kukabiliana na majanga.
Akizungumzia serikali kuhamia Dodoma, alisema kamati hiyo imeishauri itungwe sheria maalumu itakayosisitizia jambo hilo na kuongeza nguvu katika kuisimamia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) inayolalamikiwa kwa kuwa na urasimu mkubwa katika upangishaji wa ardhi.
Share:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba