Wednesday, 26 October 2016

Azam yamnyemelea Kocha Pluijm

KOCHA Hans van der Pluijm baada ya kuachana na Yanga inadaiwa kuwa huenda akatua Azam FC.
Hatahivyo, taarifa zilidai kuwa bado haijafikiwa muafaka kama kocha huyo raia wa Uholanzi atachukua nafasi ya ukocha mkuu au ile ya ukurugenzi wa ufundi, ambayo ameikataa katika klabu ya Yanga.
Pluijm alitangaza kuondoka Yanga baada ya uongozi wa klabu hiyo kufanya mazungumzo na Kocha Mkuu wa Zesco United ya Zambia, George Lwandamina ili kuifundisha timu hiyo.
Lwandamina amemalizana na Yanga na aliondoka kurudi kwao Zambia kabla ya kurudi tayari kuinoa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani jijini Dar es Salaam.

Lakini Azam FC imeonesha nia ya kumnasa Pluijm ambaye iliwahi kumuwania hapo awali.
“Kuna mazungumzo ingawa inafanywa siri kubwa, sijajua sahihi ni mkurugenzi wa ufundi au kocha mkuu.
“Nafikiri ni suala ambalo linaendelea kushughulikiwa,” kilieleza chanzo chetu hicho.
Kumekuwa na ugumu kuwapata viongozi wa Azam FC lakini juhudi zinaendelea ili kupata kauli yao kuhusiana na Pluijm pia Kocha Zeben Hernandez raia wa Hispania ambaye anakinoa kikosi hicho.
Pluijm alipoulizwa jijini Dar es Salaam jana alisema kwa mkato kuwa sio kweli na wala hawezi kulizungumzia hilo.
Share:

NIT yatakiwa kuboresha ukaguzi magari

CHUO cha Usafirishaji Tanzania (NIT) jijini Dar es Salaam kimetakiwa kuboresha idara yake ya ukaguzi wa magari kwa ajili ya kukijengea uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, Profesa Norman Sigalla baada ya kamati hiyo kusikiliza na kujadili taarifa ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu utendaji kazi wa NIT na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Ameitaka wizara hiyo kusimamia maboresho ya miundombinu kwenye vyuo vya NIT na DMI ili viwe na hadhi kulingana na umuhimu wake kwa taifa.
"Tunataka vyuo hivi viwe na wataalamu wenye uwezo kabla ya kupewa haki ya kufundisha ili viweze kuzalisha wataalamu wazuri wakiwemo mabaharia watakaochangia maendeleo na watakaoweza kujiajiri," amesisitiza.
Ametoa changamoto kwa vyuo hivyo vijikite kwenye utafiti na kutoa machapisho yenye lengo la kutatua matatizo yanayolikabili taifa.
“Kamati inahitaji taarifa iliyokamilika ya ujenzi wa reli ya kati katika kipindi cha kuanzia sasa na Novemba 14, mwaka huu, tumeiagiza wizara itekeleze agizo hili,” amesema.
Share:

Tuesday, 25 October 2016

TSN kubadilisha mtambo wa uchapishaji

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) imesema imejipanga kujiendesha kwa faida, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mtambo wa uchapishaji ili kuleta ushindani kwenye soko. Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alisema hayo jana wakati akihojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji mjini Dodoma.
“Kimsingi, sisi ni wafanyabiashara, tunajipanga katika kuhakikisha tunafanya biashara kiufanisi zaidi,” alisema Dk Yonazi na kuongeza kuwa, mwenendo wa kampuni kimapato umekuwa ukitegemea matangazo.
Soko kuu la TSN linategemea wizara, mashirika ya umma na kumekuwa na ushindani mkubwa. Alisema ushindani huo wa kibiashara, umechangia kubuni na kuanzishwa Kitengo cha Habari za Mtandao ili kuhakikisha wasomaji wanapata habari kila zinapotokea.
Alisema japo kumekuwepo na changamoto nyingi, wataendelea kujitahidi ili kufikia malengo waliyojiwekea kwa kushirikiana na wasambazaji na wauzaji ili magazeti hayo yafike sokoni kwa wakati na kuongeza mauzo.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili kampuni hiyo, alisema kumekuwa wadaiwa sugu, ambao wanawapitia kuona ni namna gani madeni hayo yatalipwa.
“Wadaiwa wakubwa ni serikali na taasisi zake, tumekuwa tukifuatilia, baadhi ya taasisi zimeonesha kuwa zinapitia changamoto ya kifedha na tumekwenda hadi hazina, lengo likiwa ni kuhakikisha madeni yanalipwa,” alisema na kuongeza kuwa, walikwenda hadi Zanzibar na wameahidiwa kuwa kuanzia mwezi ujao, wataanza kulipa.
Aidha, alisema kampuni hiyo inamiliki majengo mawili; moja lipo Mtaa wa Samora na Tazara jijini Dar es Salaam, na sasa wanakusudia kufanya uwekezaji mkubwa mkoani Dodoma, ambapo watajenga jengo la kisasa litakalokuwa na ofisi kwa ajili ya kupangisha.
Pia alisema wanakusudia kuingia katika soko la Afrika Mashariki na Kati na wameshaingia makubaliano na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) ili wauze Kiswahili nchi zinazoizunguka Tanzania. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Albert Obama wakati umefika kampuni hiyo kufanya mabadiliko ili ijiendeshe kwa faida.
“Punguzeni watu ili uwe na menejimenti ambayo unaimudu,” alisema Obama.
Katika michango yao, wabunge walihoji kwa nini waandishi wa mikoani hawaajiriwi, namna gani kampuni imejipanga kutoa taarifa kupitia mtandao na ina wafanyakazi wangapi, kwa sababu imekuwa ikilalamika kwamba ina ukosefu wa fedha wakati ina mlolongo wa mameneja wapatao 10 wanaongozwa na Mhariri Mtendaji.
“Mlolongo huo wa mameneja ni lazima uwe tatizo kubwa kwenye matumizi, kwani kila kitengo kinakuwa kinajitegemea. Nahitaji bajeti ionekane, mnajiendesha kwa mfumo wa kiserikali na si wa kibiashara,” alihoji Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM).
Awali katika taarifa yake, ilielezwa kwamba kampuni hiyo kwa asilimia 99 inamilikiwa na serikali kupitia kwa Msajili wa Hazina na Mkurugenzi Mtendaji anamiliki asilimia moja. Kampuni hiyo inachapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo na SpotiLeo, pia inamiliki kiwanda cha uchapishaji.
Share:

Walimu 4 watumbuliwa tuhuma za mapenzi

WALIMU wanne wa Shule ya Sekondari Kitumbeine wilayani Longido Mkoa wa Arusha, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wao.
Akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye yupo wilayani humo kwa ziara ya siku tano ya kukagua maendeleo na changamoto, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema hivi sasa uchunguzi unafanyika, kubaini jinsi walimu hao walivyojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.
Chongolo alisema uchunguzi utakapokamilika na ikithibitika, watachukuliwa hatua za kinidhamu. Alisema pia kuwa kuna changamoto ya mimba ya utotoni, ambazo baadhi ya wazazi na walezi wao wamekuwa wakiwaozesha kutokana na mila.
Alisema serikali inafuatilia wazazi wenye tabia hiyo ya kuwaozesha watoto kwenye umri mdogo kwani tatizo hilo lipo kwa asilimia 13 katika jamii ya wafugaji.
Hata hivyo, alisema mimba za utotoni zimepungua kutoka sita mwaka 2013 na kufikia nne ingawa bado kuna changamoto ya wasichana kuozeshwa kwenye umri mdogo na wazazi wao.
"Tupo kwenye uchaguzi ili kubaini kama kweli walimu hao wamehusika na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao au la na endapo ikithibitika kuhusu hilo hatua kali za kinidhamu zinafanyika," alisema bila kuwataja majina wahusika hao.
Aidha, alisema wilaya hiyo pia ina upungufu wa miundombinu ya madarasa 128, nyumba za walimu 281, matundu ya vyoo 393 na madawati 1,320 ambapo katika mwaka huu wa fedha 2016/17 wilaya imejitahidi kujenga madarasa 60, nyumba za walimu saba pamoja na kuongeza shule za msingi sita ili kupunguza tatizo hilo. Baada ya Gambo kupokea taarifa hiyo, alishiriki kupaua bweni la Shule ya Sekondari Longido lililoungua.
Alitoa rai kwa polisi kufanya doria za mara kwa mara shuleni ili kudhibiti matatizo ya moto na kuimarisha usalama wa wanafunzi, pia wanafunzi kushirikiana kwa pamoja na walimu ili kuimarisha ulinzi nyakati za masomo ya usiku.
Alisisitiza kuwa serikali inawasaka wale wote waliohusika na kitendo cha uchomaji moto shule mbalimbali mkoani humo ili kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
Alitoa rai kwa viongozi wa vijiji, kuhakikisha wanashiriki kupanga ulinzi kwenye maeneo yao ili kudhibiti mambo mbalimbali ya uvunjifu wa amani ikiwemo suala la moto.
Share:

Wanaonunua mazao shambani kudhibitiwa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Mazingira, ikiwa ni pamoja na azma ya kuupandisha hadhi msitu wa Masingini kuwa msitu wa hifadhi.
Aliyasema hayo jana katika kikao maalumu kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambako Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Mazingira iliwasilisha taarifa yake ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa wizara hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Dk Shein alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea kuziimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutambua umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya nchi pamoja na wananchi wake.
Alisisitiza haja ya kuendeleza mchakato wa kuanzisha kiwanda cha matrekta hapa nchini kama ilivyoamua serikali, kwani tayari hatua za awali zimeshafanyika kwa kuzingatia kuwa kilimo huimarika panapokuwa na huduma za matrekta.
Alieleza kuwa, haja kwa uongozi wa wizara hiyo kuendelea na juhudi za kuulinda msitu huo ili kuepuka kuja kuvamiwa kwa ujenzi huku akitumia fursa hiyo kuitaka wizara hiyo kusimamia na kudhibiti vyema maliasili zisizorejesheka ili kuepuka athari zaidi za hapo baadaye.
Mapema Waziri wa Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa sekta ya kilimo inajumuisha sekta ndogo za mazao, mifugo, uvuvi na misitu bado inaendelea kuwa ni mhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar na inatoa mchango wa moja kwa moja katika kujikimu kimaisha.
Alisema sekta hiyo imekuwa ikitoa ajira rasmi kwa asilimia 40 na zaidi ya asilimia 70 ya wananchi, wanategemea sekta hiyo kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana Julai hadi Septemba mwaka huu, ni pamoja na kuongeza idadi ya wafugaji wa ng'ombe wa kisasa, kufundisha mabwana mifugo, kuimarika huduma za ugani, kuongezeka kwa uzalishaji wa mayai, kuendeleza miundombinu ya utafiti na mengineyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd aliipongeza wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpangokazi wake na kusisitiza haja ya kuendelea na mikakati ya kudhibiti misumeno ya moto kwa mashirikiano ya pamoja.
Share:

Maegesho ya magari kukamua wakazi Dar

ALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Sipora Liana imejipanga kukusanya jumla ya Sh bilioni saba kwa mwezi kutoka Sh milioni 103 za sasa kupitia maegesho ya magari katika jiji hilo.
Liana amesema jana mjini Dodoma kuwa, tayari wametangaza zabuni kwa manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke baada ya kufanya tathmini ya maegesho yote jijini humo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Liana amesema kwa tathmini ya awali, Manispaa ya Temeke inatarajiwa kukusanya jumla ya Sh milioni 680, Ilala Sh bilioni 4.6 na Kinondoni Sh bilioni 1.9 ifikapo Novemba Mosi, mwaka huu.
Amesema halmashauri hiyo ilikuwa inakusanya Sh milioni 73 kwa mwezi ambayo imepanda na kufikia Sh milioni 103 kwa muda wa miezi miwili tu. Hata hivyo, mkurugenzi huyo alijikuta katika hali ngumu baada ya wajumbe wa kamati hiyo kumbana kuhusu hesabu za halmashauri ya jiji hilo za mwaka wa fedha 2014/15.
Awali, almanusura halmashauri hiyo itimuliwe kwenye kikao hicho baada ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Teresia Mbando kutohudhuria bila kutoa taarifa.
Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliahirisha kujadili hesabu za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na kuagiza RAS huyo awe amewasili mjini Dodoma leo asubuhi ndio itaendelea na shughuli zake za kamati.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota alimtaka Katibu Tawala wa Serikali za Mitaa na Kaimu RAS, Mary Yassin kueleza mbele ya kamati hiyo mahali alipo Mbando kwa kuwa taarifa zote za alipo Katibu Tawala huyo kamati hiyo inazo.
"Wajumbe nasema hivi kwa sababu, RAS wa Dar es Salaam alishajiandaa kuja kwa safari hii na alishatoka nyumbani kwake, taarifa tunazo, naagiza hapa kesho (leo) awe amewasili mbele ya kamati hii tuendelee la sivyo hatutovumilia kamati yetu kudharauliwa,” amesisitiza.
Aliitaka Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iwasilishe ujumbe kwa viongozi wote wa serikali za mitaa kuwa kamati hiyo, kamwe haijaribiwi kwani ina mamlaka kamili ya Bunge kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema kiongozi huyo wa jiji amekiuka Kanuni za Bunge ya Haki, Kinga na Maadili kwa kutowasilisha taarifa za kutodhuria kwake kwenye kamati hiyo.
“Inawezekana RAS na baadhi ya wenzake wengine, wanafikiria kamati ni kama kikundi cha watu tu wamejikusanya, napenda waelewe kuwa hili ni Bunge na Bunge lina sheria. Kilichotokea huku ni kwenda kinyume cha Sheria ya Haki, Kinga na Maadili na RAS amelidharau Bunge”.
Kaimu RAS wakati akijitetea alibainisha kuwa hana barua ya kumkaimisha nafasi hiyo ya Katibu Tawala, ingawa kwa mujibu wa cheo chake alilazimika kumuwakilisha.
Share:

Rooney aandika rekodi mpya kucheza michezo England

Wayne Rooney ameandika historia ya kuwa mchezaji aliyeichezea timu ya taifa ya England mara nyingi zaidi, kwa wachezaji wa ndani ya uwanja.
Ulikuwa mchezo wake wa 116 kuiwakilisha England alipocheza na Slovakia katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia la mwaka 2018.
Rekodi hii inaipita ile ya David Beckham ambaye aliichezea timu ya Taifa la England mechi 115.
Share:

Wafanyabiashara wakumbushwa kutafuta masoko nje

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kutumia fursa ya gharama nafuu za usafiri wa anga, kutafuta masoko nje nchi.
Mwito huo ulitolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fastjet, Nico Bezuidenhout wakati akizungumzia ushirikiano kati ya Fastjet na kampuni ya Amedeus inayojihusisha na teknolojia ya hali ya juu katika sekta ya usafiri wa anga duniani.
Alisema kuwa kutokana na kampuni hiyo kuwa na mtandao mkubwa wa biashara za anga duniani wafanyabiashara hao kama wateja wengine watanufaika na gharama nafuu za usafiri.
“Ushirika wetu na Amadeus kampuni ambayo ina mtandao mkubwa duniani wa wakala wa usafiri na idara ya usafiri ya kampuni ni maendeleo makubwa kwa fastjet ambayo yanatuwezesha sisi kupanua mtazamo wetu wa kufika maeneo mengi,” alisema ofisa huyo.
Aliongeza kuwa wanatarajia kuona ongezeko kubwa la ukataji wa tiketi katika biashara ya usafiri ndani ya mtandao wao.
Bezuidenhout alisema mawakala wa usafiri watakata tiketi na kulipia safari za fastjet kwa wateja wake kupitia Amadeus na kwamba chini ya mfumo huo mteja wakiwemo wafanyabiashara waliokata tiketi zao kupitia Amedeus watanufaika na ofa ya kusafirisha begi moja la kilo 20.
Share:

Marufuku kuagiza migomba Msumbiji

TANZANIA imepiga marufuku uingizaji migomba na mazao yake kutoka Msumbiji kwa kuwa nchi hiyo imekumbwa na ugonjwa unaoshambulia zao hilo ambao kitaalamu unajulikana kwa jina la Panama Disease.
Haya yalisemwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa afya ya mimea kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia afya ya mimea katika wizara hiyo, Cornelius Mkondo.
Dk Turuka alisema katika kuhakikisha mazao ya migomba hayaingii nchini kutoka Msumbiji, Tanzania imeweka wataalamu wake wa mimea katika mipaka na nchi hiyo, viwanja vya ndege na maeneo yote muhimu ili kuimarisha ukaguzi.
Alisema ugonjwa huo haujaingia nchini, lakini tayari wamechukua tahadhari kwa kuzuia uingizwaji wa mazao ya migomba kutoka Msumbiji kwa kuwa ugonjwa huo ni hatari.
Mbali na ugonjwa huo, pia Tanzania kwa sasa haiwezi kusafirisha matunda kwenda Afrika Kusini kutokana na kuwepo mdudu hatari wa matunda.
Dk Turuka amewaambia washiriki wa mkutano huo unaoshirikisha nchi 15 za SADC na COMESA kuwa mkutano huo ni muhimu katika kupanga mikakati ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mimea katika ukanda wa Afrika kwani magonjwa hayo katika sekta ya kilimo yanaathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na uchumi wa nchi na wananchi wake na kusababisha kukosekana kwa uhakika wa usalama wa chakula na mazao.
Ugonjwa wa migomba huathiri uzalishaji kwa asilimia 70 katika nchi za SADC na husababisha hasara ya tani 1.52 za ndizi katika nchi hizo.
Pia alisema ugonjwa wa mahindi uliozikumba nchi za Afrika Mashariki ulitokea kuwa ugonjwa hatari na kuathiri zaidi uzalishaji wa mahindi na kutishia usalama wa chakula kwa kaya nyingi.
Share:

RC aagiza mlinzi alipwe mishahara ya miezi 22

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Bosco Ndunguru, kulipa malimbikizo yote ya mishahara ya miezi 22 yanayofikia Sh 660,000 ya mlinzi wa Shule ya Msingi Ndevelwa, Agustino Paul (58), badala ya kuendelea kumpiga danadana.
Mwanri alitoa agizo hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Ndevelwa iliyopo katika manispaa hiyo baada ya mkuu huyo wa mkoa kuhutubia wananchi na kutoa nafasi ya kuuliza maswali au kueleza kero zao.
Baada ya mlinzi huyo kutoa malalamiko yake, Mwanri alimwita Mtendaji wa kata hiyo Hamis Kasonta ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo, ambapo alikiri mlinzi huyo kutolipwa mishahara yake na uongozi wa shule hiyo ya serikali kwa miezi 22.
Diwani wa kata hiyo, Seleman Maganga, alieleza kuwa awali mlinzi huyo alikuwa anapata mshahara wake kama kawaida, lakini baadaye wakaacha kumlipa kwa kisingizio cha serikali ya kijiji kutopokea fedha yoyote ya uwezeshwaji kutoka halmashauri ya manispaa.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Chatta Lukela, alisema suala hilo lipo chini ya uongozi wa shule na serikali ya kijiji ndio inayopaswa kumlipa mishahara yake yote mlinzi huyo.
Baada ya maelezo hayo, Mwanri alisema kwa kuwa serikali ya kijiji haijapata mgao wa fedha za uwezeshwaji kutoka halmashauri ya manispaa, deni hilo lilipwe moja kwa moja kutoka ofisi ya mkurugenzi wa manispaa na utaratibu wa malipo uanze mara moja hata kama ni kidogo kidogo.
Ili kuhakikisha deni hilo linalipwa, Mwanri alimwagiza mkuu wa wilaya ya Tabora, Queen Mlozi kulisimamia na kumpa mrejesho wa kufanyika kwa malipo hayo.
Akizungumza mlinzi huyo, alisema alianza kazi hiyo mwaka 2014 kwa makubaliano ya kulipwa Sh 30,000 kwa mwezi na alilipwa miezi kadhaa lakini baada ya hapo hakulipwa tena ila aliambiwa avumilie fedha zikipatikana atalipwa.
"Baada ya kukaa miezi kumi bila kulipwa niliamua kuacha kazi lakini baadaye wakanirudisha tena huku wakiahidi kunilipa kidogo kidogo mpaka deni liishe, ahadi hiyo haijatekelezwa hadi leo na bado niko kazini," alisema.
Share:

Makonda: Niko tayari kumsaidia Rehema

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema yuko tayari kumsaidia Rehema Mwilu (16) ili atimize ndoto yake ya kusoma na kuwa mwalimu, baada ya kushindwa kufanya hivyo kutokana na umasikini wa wazazi wake.
Rehema ni binti anayeishi Mtoni Kijichi Dar es Salaam, alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Mtoni Kijichi mwaka 2013 na kufaulu na alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kibada.
Lakini, alishindwa kuripoti shuleni kutokana na ugumu wa maisha na shule kuwa mbali, hali iliyosababisha aendelee kukaa nyumbani hadi leo. Baada ya kukaa nyumbani kwa muda, alitokea mwanaume aliyezungumza na wazazi wake na kupeleka barua ya posa na wazazi waliridhia Rehema kuolewa, kutokana na kutokuwa na pa kwenda, lakini alikataa kwa kuwa malengo yake yalikuwa ni kusoma.
Akizungumzia suala hilo, Makonda alisema ipo haja ya kujipanga kuona ni kwa namna gani Rehema ataweza kusaidiwa kusoma na kutimiza ndoto zake na aweze kusoma shule ya kulala ili kuepuka usumbufu.
“Ni kweli anahitaji msaada, lakini nitajitahidi kuweka mkakati ambao utamsaidia ili mwakani aanze shule na sio shule ya kutwa kama ilivyokuwa ile aliyochaguliwa, ni vyema atafutiwe shule ya kulala ili aweze kutulia huko na asome kukidhi matakwa yake,” alisema Makonda.
Alisema kama atasoma shule ya kutwa, itamfanya akumbane na changamoto mbalimbali, kama vile kutafuta usafiri wa daladala kwenda shule na kurejea nyumbani na pia inaweza kuwa ni gharama zaidi ya kusoma shule ya bweni.
“Ni kweli aliweza kuhimili changamoto hizo kwa miaka mitatu, lakini ili aweze kutimiza kiu yake ya kusoma ni vyema kwenda shule ya bweni,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa kama atakuwa tayari, awasiliane naye kwa kusaidiwa na gazeti hili. Hata hivyo, Makonda alisema yapo mambo mengi katika jamii, yanayochangia watoto kushindwa kutimiza malengo yao, ikiwa ni pamoja na kuwepo wenye mfumo dume, wakiamini sio vyema kwa mtoto wa kike kusoma na umaskini, ambao husababisha wazazi kuwaozesha watoto wao.
Alisema kwa upande wa Rehema, yumkini hawakutoa taarifa hata kwa uongozi wa mtaa na ni vyema kutambua kuwa kusema ndio sehemu sahihi ya mwenye kutafuta msaada kuweza kusaidiwa.
Kwa miaka yote mitatu, Rehema amekuwa nyumbani, akiwaza kuwa ipo siku atasoma na hiyo ni moja ya sababu ya yeye kukataa kuozwa, kwa kuwa anaamini ipo siku atasoma na elimu hiyo itakuwa mkombozi kwake. Katika kuhakikisha anatimiza ndoto hiyo, Rehema alipiga simu na kuwasiliana na viongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali ya TSN katika gazeti hili, akiamini kuwa kiu yake ya elimu itafanikiwa.
Kwa upande wa Ofisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara ya Maendeleo ya Watoto, Anna Mhina alisema wameisoma taarifa za Rehema na wanafuatilia suala hilo, kuhakikisha anaendelea na masomo.
Walilishukuru gazeti la HabariLeo kwa kuandika habari hiyo. Alisema kama kuna suala la kuozeshwa, atawasiliana na Mkuu wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) ili na yeye ahusishe dawati la jinsia, kuona hatua zinazoweza kuchukuliwa.
Share:

Katibu Fedha akwamisha mjadala hesabu za PSPF

KAMATI ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), imeshindwa kupitia hesabu za Mfuko wa Pensheni wa PSPF na kulazimika kuahirisha kikao chake, baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James kushindwa kuhudhuria kikao cha kamati hiyo bila kutoa taarifa.
Katibu Mkuu huyo ndiye alipaswa kwenda mbele ya kamati hiyo na viongozi wa mfuko huo kwa kuwa PSPF haina bodi na kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, zinataka shirika ambalo halina bodi, Katibu Mkuu anayewakilisha serikali kufika mbele yake.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka, alisema kamati imesikitishwa na kitendo cha Katibu Mkuu huyo na kubainisha kuwa wajumbe, wamekitafsiri kama ni dharau kwa kamati hiyo na Bunge.
"PAC haitaki dharau na kuburuzwa kwa sababu inajulikana wazi kuwa katibu huyo alipewa taarifa ya kuhudhuria kikao hicho na kuthibitisha kuwa atahudhuria, lakini hakufika bila kutoa taarifa yoyote,” alisema Kaboyoka.
“Tunajua hili si kosa lenu, ila Katibu Mkuu amewaponza. Naagiza Katibu Mkuu huyu afike mara moja kesho afike kwenye kamati bila kutuma mwakilishi,” alisisitiza.
Alisema hali ya mfuko huo hairidhishi kwani dalili zinaonesha kuwa, unakaribia kufa kutokana na kuelemewa na madeni ambayo mengi kati yake unaidai serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema mahudhurio ya katibu huyo katika kamati hiyo ni muhimu kwani anapaswa kujibu namna serikali itakavyouokoa mfuko huo kutokana na kuendelea kuwa katika hali mbaya ya kifedha.
Share:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba