Wednesday 2 November 2016

Tanzania yaipa somo ICC kukabili mpasuko

WAKATI nchi kadhaa za Afrika zikionesha dalili za kutaka kujiengua kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Tanzania imeishauri mahakama hiyo kukaa meza moja na nchi wanachama wa Mkataba wa Roma, hasa za Afrika ili kutafuta suluhu ya changamoto na tofauti zilizopo kati ya mahakama hiyo na wanachama wake.
Imetoa mwito huo mwanzoni mwa wiki hii kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Tuvako Manongi wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopokea na kujadili taarifa ya utendaji wa ICC. Alisema uwepo au kuanzishwa kwa ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji mkono kutoka nchi za Afrika.
Alisema uungwaji mkono huo ulisababishwa na namna nchi hizo za Afrika zilivyokatishwa tamaa na kuvunjika moyo baada ya kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
“Baada ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo, mahakama hii, ilikuja kuwa chombo cha kutenda haki dhidi ya watu waliojihusisha na vitendo vya kikatili vikiwamo vya ukatili dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,” alisema Balozi Manongi.
Alisema kutokana na madhara makubwa yasiyoelezeka yaliyotokea Afrika yaliifanya mahakama hiyo kuwa chombo cha matumaini dhidi ya wale ambao hawakuweza kuguswa au walikuwa juu ya sheria.
“Tanzania inatambua kuwa uhusiano kati ya mahakama hii na Afrika ni ule wa misuguano, na ni uhusiano ambao umeleta hofu ya Afrika kujitoa,” alisema na kuongeza kuwa hofu hiyo ya kujitoa kwa Afrika katika mahakama hiyo, haipaswi kuwepo kutokana na mambo kadhaa ambayo Afrika imejipanga kuyatekeleza kwa manufaa ya bara hilo na watu wake.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika maarufu kama agenda 2063 ambayo pamoja na mambo mengine inachagiza katika utawala bora, demokrasia, usawa wa jinsia, kuheshimu haki za binadamu, haki na utawala wa sheria.
“Viongozi wa wakuu wa nchi na serikali wa Afrika wameutangaza mwaka 2016 kuwa mwaka wa haki za binadamu huku mkazo ukielekezwa katika haki za wanawake. Na katika kutambua kuwa Amani na Haki ni vitu visivyoweza kutenganishwa, kwa sababu hizo, tunachotakiwa kuhimiza leo sana sana ni majadiliano,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Tanzania imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutopeleka ICC rufaa zenye mlengo wa kisiasa, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuharibu sifa ya ICC na kuifanya isiaminiwe na kuonekana inatumiwa na wakubwa kutimiza malengo yao.
Taarifa ya ICC iliwasilishwa na Rais wa mahakama hiyo, Jaji Silvia Fernandez de Gurmendi katika kipindi ambacho Jumuiya ya Kimataifa imekumbwa na taharuki baada ya wanachama wawili Afrika Kusini na Burundi kuwasilisha rasmi UN kusudio la kujiondoa huku Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa haijawasilisha rasmi nia yake hiyo.
Share:

0 comments:

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba

nunua vitabu vya watoto kuanzia chekechekea mpaka darasa la saba