Lowassa ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu, alifika jana saa 2:40 katika viwanja vya Bunge na kutumia dakika kadhaa kusalimiana na baadhi ya wabunge nje ya ukumbi kabla hajaingia ndani.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu ujio wake bungeni, Lowassa, aliyekuwa Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM kwa takribani miaka 20 hadi mwaka jana alipohamia Chadema, alisema yupo Dodoma kwa shughuli za chama chake. “Nimekuja kwa ziara, nikishatambulishwa huko ndani, nitaongea si sasa,” alisema Lowassa aliyepokewa na wabunge wa vyama mbalimbali, wakimsalimia na wengine wakimsindikiza katika lango la kuingilia katika ukumbi wa Bunge kufuatilia shughuli za Bunge la 11.
Baadhi ya wabunge aliozungumza nao ni pamoja na Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM) ambaye alimsalimia na kumkaribisha bungeni, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), wa Bukoba Mjini, Wilfred Rwakatare (Chadema).
Baada ya kuzungumza naye kwa muda mfupi, walionekana wakijumuika wote kumsindikiza katika lango kuu la Bunge kuingia bungeni.
Ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mwenyekiti wa Kikao cha Bunge, Najma Giga, akitambulisha wageni, alimtambulisha Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Lowassa kuwa ni wageni wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.
Mbali na Lowassa na Sumaye, wageni wengine wa Mbowe walikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Profesa Abdallah Safari na Mjumbe mwingine wa Kamati Kuu, Arcado Ntagazwa.
Hata hivyo, baada ya Lowassa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wengi walisalimiana naye bila kujali itikadi zao za vyama na wengine walionekana kuteta kwa muda mrefu.
Wageni wengine waliofika na kutambulishwa ni pamoja na Rais mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella ambaye wabunge wa CCM walimshangilia kwa nguvu zote huku wa upinzani nao wakimshangilia pamoja na Balozi wa Rwanda nchini.
0 comments:
Post a Comment