SERIKALI imepanga kutumia Sh trilioni 32.946 katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018, ikiwa imeongezeka kutoka Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/2017 na kutaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na kuzingatia miradi ya kufufua kiwanda cha General Tyre cha Arusha na kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo.
Sambamba na hilo, serikali imebainisha mikakati yake ya kudhibiti matumizi, ambapo sasa itahakikisha mikataba inayoingiwa na serikali na taasisi zake inakuwa katika shilingi za Tanzania, isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara za kimataifa.
Kuhusu kuhamishia shughuli za makao makuu ya serikali Dodoma, mipango ya ujenzi wa majengo na miundombinu yote ya serikali iliyopangwa kujengwa Dar es Salaam, itahamishiwa Dodoma.
Akiwasilisha bungeni jana mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kati ya Sh trilioni 32.946, Sh trilioni 19.782 zitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
“Sh trilioni 7.206 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na Sh trilioni 9.723 ni kwa ajili ya kulipia deni la Taifa lililoiva. Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 13.164 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ambapo fedha za ndani ni Sh 9.960 sawa na asilimia 76. Kiwango hiki ni ongezeko la Sh trilioni 1.343 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017,” alifafanua.
Alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 20.872 sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote.
Kati ya mapato hayo serikali inatarajia kukusanya mapato ya kodi ya Sh trilioni 18.097 sawa na asilimia 87 ya mapato ya ndani.
Hata hivyo, alisema kiasi hicho ni makisio ya awali ambapo makisio ya mwisho yatapatikana baada ya kukamilika kwa tathmini ya nusu mwaka 2016/2017 pamoja na taarifa ya kikosi kazi cha maboresho ya kodi, kinachojumuisha wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Akizungumzia jinsi ya kudhibiti matumizi ya serikali, Dk Mpango alisema serikali itaendelea kupunguza gharama na matumizi yasiyokuwa ya lazima ikiwemo sherehe za kitaifa, posho za vikao, uchapishaji wa fulana, kofia, mikoba, safari za nje, mafunzo ya muda mfupi nje nchi na ununuzi wa samani kutoka nje.
Pia kutoa kipaumbele kwa taasisi za umma na zile ambazo serikali inamiliki hisa katika kununua huduma kama vile bima, huduma za fedha, usafirishaji wa barua, wavuti, simu, mizigo na vifurushi, matangazo na usafiri.
Waziri alitaja mikakati mingine ni kudhibiti utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vikuu kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo pekee ndio wananufaika na mikopo hiyo na kudhibiti ulipaji mishahara kwa watumishi wanaostahili pekee.
Vilevile kutumia utaratibu wa ununuzi wa nyumba kwa utaratibu wa kulipia kwa awamu hususan kwa majengo ya balozi na wawakilishi walioko nje ya nchi, badala ya kupanga na kudhibiti safari za nje ya nchi na ukubwa wa misafara.
Katika kufanikisha ukusanyaji mapato, waziri huyo aliwataka maofisa masuuli wote nchini kuweka mazingira wezeshi katika kufanikisha hilo kwa kuingia mikataba na wazabuni na makandarasi na watoa huduma wanaotumia mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFDs) na kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa vituo vya ukusanyaji mapato kama bandari, mipakani na viwanja vya ndege.
Dk Mpango alisema maofisa hao, pia wanaagizwa kufanya mapitio ya mikataba yote iliyopewa misamaha ya kodi ili kutathmini faida zake na kujipanga upya, ambapo pia kutoingia mikataba inayohusisha misamaha ya kodi bila idhini ya Waziri wa Fedha na Mipango.
Baadhi ya maeneo ya vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2017/2018 alivyotaja Dk Mpango ni miradi ya kukuza viwanda na uchumi ikiwamo miradi ya magadi Soda kwenye bonde la Engaruka, kukifufua kiwanda cha General Tyre, uendelezaji wa eneo la viwanda vidogo(Sido) katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha.
Pia bandari kavu mkoani Pwani, bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga pamoja na mradi ya makaa ya mawe Mchuchuma, chuma cha Liganga na ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam –Tabora- Kigoma kwa standard gauge na matawi yake.
0 comments:
Post a Comment